NEWS

Monday 11 March 2024

WWF Tanzania yakutanisha wadau kutathmini utekelezaji Mradi wa Uhifadhi Dakio la Mto Mara




Na Christopher Gamaina, Musoma
---------------------------------------------


SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania limewakutanisha wadau wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara katika kikao cha kupeana mrejesho wa utekelezwaji wa shughuli za mradi huo.

Pia kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2024 na kupendekeza njia sitahiki za kuboresha utekelezaji wa mradi huo.

Kikao hicho cha siku mbili kimeanza leo Machi 11, 2024 mjini Musoma, washiriki wakiwa ni kutoka Halmashauri za Wilaya, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Ofisi ya Afisa Tawala Mkoa, taasisi zisizo za kiserikali na jumuiya za watumia maji.

Washiriki wengine ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), waandishi wa habari na WWF Tanzania.


Kikao kimeanza kwa washiriki kupitishwa kwenye taarifa fupi ya mradi iliyowasilishwa na Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Christian Chonya ambaye amesema mradi huo ni wa miaka mitatu inayoishia Aprili 2025 na unafadhiliwa na USAID/ Tanzania.

Aidha, Mhandisi Chonya ametaja lengo mahsusi la mradi huo kuwa ni kusaidia kutatua changamoto za usalama wa maji na kustahimili mabadiliko ya tabia nchi yaliyopo na yanayoongezeka miongoni mwa jamii.


Kisha washiriki walipewa nafasi ya kuwasilisha taarifa fupi za utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mazingira, hususan upandaji miti, utunzaji misitu na vyanzo vya maji katika maeneo yao ya uongozi, pamoja na majadiliano ya jumla.

Kwa mujibu wa Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Mafunzo kutoka WWF, Enock Edward Rutaihwa, jukumu kubwa la Shirika la WWF ni kusaidia kwa kuunga juhudi za LVBWB katika kuwezesha wadau kutekeleza mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages