NEWS

Wednesday 3 April 2024

Benki ya Azania yadhamini hafla ya Futuru na Mama Samia wilayani Serengeti, yatangaza ukombozi kwa wanawakeMkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Dkt Rhimo Simeon Nyansaho akikabidhi msaada wa vyakula kwa watu wasiojiweza wakati wa hafla ya Futuru na Mama Samia wilayani Serengeti jana Aprili 2, 2024.
------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Serengeti
---------------------------------------


BENKI ya Azania Tanzania imedhamini hafla Futuru na Mama Samia, na kugawa msaada wa vyakula mbalimbali kwa makundi maalum, yakiwemo ya watu wasiojiweza, wenye ulemavu na watoto yatima wilayani Serengeti, Mara.

Hafla hiyo ambayo iliandaliwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ambaye amehamishiwa Mwanza, ilifanyika kwenye ukumbi wa Kisare mjini Mugumu jana Aprili 2, 2024, ambapo viongozi mbalimbali waliishukuru benki hiyo kwa udhamini ilioutoa kufanikisha tukio hilo.

RC Mtanda aliishukuru Benki ya Azania na wananchi wa Serengeti waliojitokeza kushiriki katika hafla hiyo ya aina yake.


RC Mtanda akizungumza katika hafla hiyo.
-----------------------------------------------

“Nawashukuruni sana Benki ya Azania, nilipiga simu kwa Mkurugenzi akaniambia nipe namba ya akaunti - akanipa milioni tano, akaniambia nenda ukafuturu na watu wa Serengeti.

“Kufuturisha ni kujenga mahusiano baina ya binadamu, ni maagizo ya Mwenyezi Mungu kuwakumbuka na kufuturisha wasio na uwezo, Nyansaho [Mkurugenzi wa Maendeleo wa Benki ya Azania] ni mtiifu kwa mamlaka nikupongeze sana,” alisema RC Mtanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania Tanzania, Dkt Rhimo Simeon Nyansaho alisema anatambua umuhimu wa kufunga, kufanya maombi na kusaidia watu wenye uhitaji katika jamii.

“Chanzo cha mfungo ni kufanya maombi ambayo yanasababisha utulivu, amani na upendo katika nchi, ni muda wa kuwafikiria wale wasiojiweza,” alisema Dkt Nyansaho ambaye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).


Dkt Nyansaho akizungumza 
katika hafla hiyo.
-----------------------------------------------

Aidha, Dkt Nyansaho alitumia nafasi hiyo pia kutangaza mpango wa Benki ya Azania wa kuwakomboa wanawake dhidi ya mikopo isiyo rafiki.

“Tumekuja na ‘product’ inaitwa Mwanamke Hodari baada ya kufanya utafiti, akina mama wana changamoto ya mikopo maarufu kama kausha damu yenye riba kubwa ya asilimia tano mpaka kumi kwa mwezi, sisi kama taasisi tunachoomba endeleeni kutuunga mkono,” alisema.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Serengeti, Juma Simba aliishukuru Benki ya Azania na kuhimiza makundi ya wanawake na vijana kutumia fursa za mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na benki hiyo.

“Akina mama ni wakati wa kusonga mbele kwa mikopo ya Azania, vijana ni wakati sasa wa kwenda benki ukajieleza wakakupa muongozo, ukiufuata utatoka kwenye hali ngumu na kupiga hatua moja mbele,” alisema Sheikh Simba.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages