Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka.
----------------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
-----------------------------
MKUU wa Wilaya (DC) ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka amesema hajazuia misaada ya madawati, bali ameelekeza utaratibu wa kiserikali wa kuyasambaza kwenye shule zenye uhitaji.
“Sijazuia misaada ya madawati na kamwe hatutazuia misaada kwenda kwenye taasisi za serikali wilayani Rorya, tulichofanya ni kuweka utaratibu ulio rafiki, kwamba mdau lazima akabidhi msaada kwa DC ili naye amkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya kusambaza - maana yeye ndiye anajua maeneo yenye uhitaji,” Chikoka ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo Ijumaa.
DC Chikoka alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii tangu jana, ikidai kuwa amemzuia Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Sango Kasera kutoa misaada ya madawati kwa ajili wanafunzi wa shule mbalimbali wilayani Rorya.
“Siyo kwamba amezuiwa kuleta misaada, hapana. Kwanza alishaleta tumepokea madawati 160 tumemshukuru, tumempongeza, lakini sasa ilikuwa ni jukumu la mkurugenzi kuyasambaza kwenye taasisi kwa sababu yeye ndiye anajua penye changamoto ya madawati, huo ndiyo utaratibu unaotakiwa kufuatwa.
“Ukiruhusu kila kitu kiende moja kwa moja, zinaweza zikapelekwa bidhaa ambazo zina madhara kwa watoto wetu. Kwa hiyo tumemwelekeza afuate utaratibu baada ya kuona anakwenda kwenye hizo taasisi yeye mwenyewe binafsi jambo ambalo sidhani kama lina afya,” amesisitiza Chikoka.
Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Sango Kasera kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi juu ya suala hilo.
No comments:
Post a Comment