NEWS

Saturday 6 April 2024

Aliyewahi kuwa DC Bunda, Serengeti ateuliwa CCMJoshua Mirumbe
---------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
---------------------------


KIKAO cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha mapinduzi (CCM) Taifa, kimemteua aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Joshua Mirumbe kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa chama hicho Tanzania Bara.

Kada huyo wa chama tawala - CCM amewahi pia kukaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti  kwa zaidi ya mwaka mmoja katika Serikali ya Awamu ya Nne, na kwa sasa ni mshauri wa masuala ya kilimo cha pamba.

Mirumbe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), ni miongoni mwa makada wanne walioteuliwa na kikao hicho kilichofanyika Aprili 4, mwaka huu jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi.

Wengine walioteuliwa na nafasi zao zikiwa kwenye mabano ni Ali Issa Ali (Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Zanzibar), Tunu Juma Kondo (Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania - UWT Zanzibar) na Abdi Mahamoud Abdi (Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar).

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ilisema uteuzi huo unalenga kuimarisha uhai na maendeleo ya jumuiya za chama hicho tawala.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages