NEWS

Monday, 15 April 2024

Kinana awanoa wana-CCM Rorya, asema uchaguzi ujao utakuwa wa ushindani mkali, Chandi agusia mikakati ya ushindi



Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana (wa pili kulia mbele), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (kulia) na viongozi wengine wakiwasili Shirati wilayani Rorya jana.
-----------------------------------------------

Na Waandishi Wetu
Mara Online News, Rorya
------------------------------------


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amewataka wanachama wa chama hicho wilayani Rorya kujipanga vizuri kwani uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa ushindani mkali.

"Mwaka ujao mchuano wa uchaguzi ni mkali sana, tushikamane, kama kuna mtu yuko mguu pande, chama kiwaite," alisisitiza Kinana wakati akihutubia mkutano wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mabaraza ya jumuiya za chama hicho uliofanyika Shirati wilayani Rorya jana.

Kwa upande mwingine, Kinana aliwataka wana-CCM Rorya kuepuka siasa za ukabila, vinginevyo zitawagawa na kuunda makundi yanayohasimiana.

Aliyasema hayo baada ya baadhi ya wajumbe mkutano huo kuibua hoja kwamba kuna mambo yanafanyika Rorya ambayo yanaashiria kuwepo kwa siasa za ubaguzi wa kikabila miongoni mwao.

“Usimpe mtu nafasi ya uongozi kwa sababu ya kabila lake, dini au umbile, hayo ni mambo ya kizamani sana.  alisisitiza Kinana.


Kinana akisisitiza jambo katika mkutano huo.
-------------------------------------------------

Awali, akimkaribisha Kinana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi alisema chama hicho kinaendelea kujiimarisha katika mikakati itakayokipatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.

Aidha, Chandi alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha madiwani wa CCM kuhakikisha kuwa chama hicho kinapata ushindi katika maeneo yao ya uongozi.

“Diwani atakayeshindwa kusimamia mwenyekiti wa kitongoji ashinde katika eneo lake hana nafasi ya kugombea udiwani,” alisema Chandi.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Kinana, yupo mkoani Mara kwa ziara ya kuimarisha chama hicho, ambapo ratiba inaonesha kuwa leo atakuwa wilayani Bunda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages