NEWS

Thursday, 18 April 2024

Kinana ampa Chandi rungu la kudhibiti makundi yanayojitokeza CCM Mara



Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mabaraza ya jumuiya za chama hicho jimbo la Musoma Mjini jana.
-----------------------------------------------

Na Mara Online News, Musoma
-------------------------------------------


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ameiagiza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara chini ya Mwenyekiti wake, Patrick Chandi kudhibiti makundi yanayotishia uhai wa chama hicho mkoani humo kuelekea kipindi cha uchaguzi.

“Mimi ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Usalama wa Chama Taifa, hili suala nalikabidhi kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa walimalize maana wakishindwa likija kwangu nitatoa maamuzi magumu," alisema Kinana katika mkutano wake na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mabaraza ya jumuiya za chama hicho Musoma Mjini jana.

Kwa upande wake Chandi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, aliahidi kuendelea kusimama imara katika kutatua changamoto zinazojitokeza ndani ya chama hicho mkoani humo.

Aidha, Chandi aliwashukuru mabalozi wa chama hicho kutokana na kazi nzuri waliyofanya hadi kukiwezesha chama hicho ndani ya mkoa huo kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.

“Hali hiyo imewezesha miradi mingi kutekelezwa kwa kasi chini ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Daktari Samia Suluhu Hassan,” alisema Chandi katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa CCM Musoma Mjini.

Hata hivyo, Mwenyekiti Chandi alisema kipimo cha madiwani wanaofaa kuteuliwa kutetea nafasi zao kwenye uchaguzi mkuu mwakani, ni ushindi wa wagombea wa CCM wa uongozi wa vijiji na mitaa kwenye maeneo yao ya uongozi.

Chandi alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Kinana kutokana na ziara ya mafanikio aliyoifanya ya kukagua na kuimarisha uhai wa CCM mkoani Mara, ambayo ilihitimishwa jana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages