NEWS

Thursday 25 April 2024

Kuelekea Maadhimisho Miaka 60 ya Muungano: Kamati ya Ulinzi na Usalama Tarime yafanya usafi soko la RebuMkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Mauld Hassan Surumbu (mbele) akiongoza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kufanya usafi katika soko la Rebu leo asubuhi.
--------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
------------------------------------


KAMATI ya Ulinzi na Usalama (KUU) Wilaya ya Tarime ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa Wilaya, Kanali Mauld Hassan Surumbu imefanya usafi wa mazingira katika soko la Rebu leo asubuhi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo mara baada ya kufanya usafi, Kanali Surumbu amesisitiza kuwa suala la usafi ni endelevu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu hususan kipindi hiki cha mvua.

"Tutaendelea kufanya usafi kadiri itakavyowezekana… maana maendeleo ni pamoja na usafi wa mazingira,” amesema.


Aidha, Kanali Surumbu ametumia fursa hiyo pia kusikiliza kero za wafanyabiashara katika soko hilo na kuzitolea maelekezo ya utatuzi.

Kero hizo ni pamoja na ukosefu wa taa, maji, sehemu ya kujikinga mvua na jua. Nyingine ni ‘utitiri’ wa ushuru, harufu mbaya kutokana na mlundikano wa uchafu katika soko hilo.Katika hatua nyingine, Kanali Surumbu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kupeleka wataalamu wa kuelimisha wafanyabiashara ya dagaa kuhusu mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri.

"Mkurugenzi, wiki ijayo wataalamu wanaohusika na mikopo ya asilimia kumi waje kuzungumza na wafanyabiashara wa dagaa na taarifa niipate," ameagiza.

Shughuli hiyo ya usafi itafuatiwa na mashindano ya mpira wa miguu na pete katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Tarime (TTC), kisha hafla ya mkesha kwenye uwanja wa Shamba la Bibi ambayo itahusisha kusoma historia ya Muungango, kugawa zawadi kwa washindi wa mashindano, kusikiliza na kufuatilia hotuba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages