NEWS

Monday 8 April 2024

Mamba wa mto Mara sasa wawa tishio kwa binadamu, mifugo wilayani Serengeti, TarimeMamba wakiwa majini
--------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
----------------------------------------


WANYAMAPORI aina ya mamba wameendelea kuua raia wakiwemo watoto katika mto Mara upande wa Tanzania.

Taarifa zilizopo zinaonesha wahanga wengi wa wanyamapori hao ni raia ambao wamekuwa wakivuka mto Mara kutokea wilayani Serengeti kwenda wilayani Tarime kujitafutia riziki na kufanya manunuzi ya mahitaji ya nyumbani.

Tayari watu kadhaa wakiwemo watoto wameripotiwa kuuawa na mamba wakati wakivuka mto huo, huku tukio la hivi karubuni likimhusu mzee mwenye umri wa miaka 60 aliyetambuliwa kwa jina la Grayson Nyangi, mkazi wa kijiji cha Borenga wilayani Serengeti.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Borenga, Henry Maro, mbali na kisa cha mauaji ya mzee huyo kilichotokea Machi 28, mwaka huu, siku iliyofuta mamba waliua ng’ombe kijijini hapo.

“Wananchi wetu wanaishi kwa wasiwasi, mamba wameongezeka wanakamata na kuua watu, hasa katika vijijii vya kata ya Kisaka vilivyo jirani na mto Mara,” alisema Maro katika mahojiano na Sauti ya Mara kwa njia ya simu juzi.

“Watu wanashindwa kuvuka kwenda kuuza vitu kama chakula, ng’ombe ama kununua mahitaji upande wa Tarime kwa sababu ya kuhofia mamba, tunaomba serikali itusaidie,” aliongeza.

Alisema Borenga ni miongoni mwa vijiji vilivyo jirani na mto huo ambao wakazi wake wanategema shughuli za ufugaji na kilimo, huku soko lao kubwa likipatikana upande wa Tarime.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kembambo yenye vijiji vilivyo jirani na mto Mara upade wa wilaya ya Tarime, Rashid Bogoma alisema mamba wameshaua watu wengi.

“Mamba wameua na kujeruhi watu wengi sana, hasa vijana, madhara ni makubwa, ng’ombe sasa ndio usiseme,” Bogomba ambaye ni diwani kutoka chama tawala - CCM alisema.

Wananchi hao sasa wanaiomba serikali kuona uwezekano wa kupunguza idadi ya mamba ambayo wanaamini imeongezeka katika mto huo ambao unaanzia katika milima ya Mau nchini Kenya na kupita katika mbuga ya Masai Mara (Kenya) na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

“Tunaomba maliasili wawatege hawa mamba wamekuwa wengi sana, wawapunguze mto Mara ili wasiendelee kuleta madhara,” alisisitiza Bogomba ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime.

Ombi hilo la Bogomba liliungwa mkono na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Borenga, Maro.

“Hawa mamba ni wengi, wameongezeka, tunaomba maliasili wawapunguze hawa mamba. Wanaua watu karibia kila mwaka katika vijiji vyetu, na ng’ombe ambao wanauawa na mamba ni wengi,” alisema Maro.

Madhara hayo yanaripotiwa pia kutokea katika vijiji vya upande wa Tarime vilivyo jirani na mto Mara.

Kwa mjibu wa Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan kuna umuhimu wa kupeleka elimu kwa wananchi wanaoishi jirani na mto Mara ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya mamba.

“Solution (suluhisho) ni awareness [akimanisha kutoa elimu] ili wananchi wafahamu tabia za mamba na kuchukua tahadhari,” Lendoyan aliiambia Sauti ya Mara.

Afisa huyo alikiri bila kutoa takwimu kuwa mamba wa mto huo wamesababisha vifo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.

“Mfano mwaka jana, mtoto wa miaka 11 aliuawa na mamba akiwa anachunga mifugo na mpaka leo mwili wake haujapatikana,” alisema Lendoyan.

Kuhusu kupunguza idadi ya mamba katika mto huo, Lendayon alisema ni moja ya suluhisho na kwamba ombi la kufanya hivyo lilishawasilishwa kwenye wizara husika miaka kadhaa iliyopita.

Kwa asili mamba ni wawindaji wanaojitafutia chakula kwa kuvizia wanyama, au watu wanaokwenda kunywa, kuchota maji au kuvuka mtoni.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages