
Jumanne Abdallah Sagini (aliyevaa miwani) akiwa kwenye hafla ya futari aliyowaandaliwa Waislamu na Wakristo wilayani Bunda jana.
Butiama
-----------------
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara, Jumanne Abdallah Sagini, amefuturisha watu zaidi ya 300 kutoka makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wazee, watoto, wajane na wenye mahitaji maalum.
Futari hiyo ya futari ilifanyika jana nyumbani kwa Sagini katika kijiji cha Kiabakari, kata ya Kukirango, wilayani Butiama, ambapo iliwashirikisha Waislamu na Wakristo, na kuleta maana kubwa kipindi hiki muhimu cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresima.

Aidha, futari hiyo iliambatana na ugawaji wa tende katika misikiti 16 ya wilayani Butiama, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa utamaduni wa kusaidia jamii bila ubaguzi - ambao Sagini amekuwa nao hata kabla hajawa mbunge, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na maadili katika jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Sagini aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito wa kushiriki futari ya pamoja na kusisitiza umuhimu wa kutumia kipindi cha mfungo huo kuimarisha upendo, umoja, maadili na kutenda mema.
“Ninawashukuru kwa kuitikia wito wa kujumuika nami katika Iftar ya pamoja. Nawaahidi kuendelea kushirikiana nanyi, na pia nawaomba tutumie mwezi huu mtukufu kuhimizana kufanya yaliyo mema katika jamii,” alisema Sagini.

Wananchi waliohudhuria hafla hiyo ya futari walimpongeza Sagini kwa moyo wake wa upendo na kujitoa kwa jamii, wakisema utamaduni huo wa kukutanisha watu wa makundi mbalimbali unasaidia kuimarisha mshikamano na kuendelea kuwajali watu wenye mahitaji maalum.
Waliiongeza kuwa vitendo kama hivyo vinaimarisha upendo na umoja wa wananchi wa Butiama na kuwa mfano wa namna watu wenye uwezo wanavyoweza kuendelea kuwa karibu na jamii hata wakiwa nje ya nafasi za uongozi.

No comments:
Post a Comment