NEWS

Monday 22 April 2024

Mgodi wa Barrick North Mara ulivyookoa wanafunzi wa kike kuogea nje, kubanana vitandani Sekondari ya MangaSehemu ya jengo la vyumba 12 vya bafu lililojengwa katika Shule ya Sekondari Manga kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara.
--------------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-----------------------------------------


MATATIZO ya ukosefu wa bafu na upungufu wa vitanda vya wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Manga, limebaki historia baada shule hiyo kuonja matunda ya uwepo wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wilayani Tarime.

Mkuu wa Shule hiyo, Mwl Editha Lazaro Nakei anasema kampuni ya Barrick imeipatia shule hiyo fedha zilizogharimia ujenzi wa vyumba 12 vya bafu za kisasa, na hivyo kuwaondolea wanafunzi adha ya kuogea nje.

“Fikiria wanafunzi wetu kabla ya hapo walikuwa wanaogea nje, lakini sasa bafu za kuogea ni nzuri na za kisasa. Wanaoga muda wanaopenda, sio lazima kusubiri jioni wakati wa giza,” alisema Mwl Nakei katika mazungumzo na Sauti ya Mara shuleni hapo wiki iliyopita.

Mbali na msaada wa ujenzi wa bafu hizo, Kampuni ya Barrick pia imetoa fedha ambazo zimetumika kuongeza vitanda 70 katika shule hiyo iliyopo kata ya Komaswa.

Taarifa zilizopo zinaonesha ujenzi wa bafu hizo na ununuzi wa vitanda hivyo ni sehemu ya matunda ya mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa Kampuni ya Barrick ambayo inaendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Wanafunzi pia walikuwa wanalala wawili wawili kwenye kitanda kimoja lakini sasa kila mwanafunzi analala kwenye kitanda chake,” anaongeza Mwl Nakei huku akionesha kuwa na furaha kutokana na mchango huo wa Barrick.

Wanafunzi watoa ushuhuda
Wanafunzi waliozungumza na Sauti ya Mara, waliushukuru mgodi huo wakisema mchango huo wa Barrick umewapunguzia changamoto za huduma muhimu za malazi na bafu.

“Zamani tulilazimika kubanana wanafunzi wawili wawili kwenye kitanda, tulikuwa kwenye hatari ya kuambukizana magonjwa, lakini kwa sasa tunalala mmoja mmoja. Tunaushukuru sana mgodi wa Barrick North Mara kwa kutununulia vitanda,” anasema Ester Supeti Kipetete wa kidato cha sita.

Kuhusu bafu, mwanafunzi Inyasi Lyimo anakiri kuwa vyumba 12 vilivyojengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara vimewapunguzia adha walizokuwa nazo.

“Kutokana na upungufu mkubwa wa vyumba vya bafu uliokuwepo, baadhi ya wanafunzi tulikuwa tunalazimika kutumia vyumba vya choo kuoga, na wakati mwingine tulilazimika kuogea nje, lakini tangu Barrick watujengee bafu 12 adha zimepungua,” anasema Inyasi anayesoma kidato cha sita pia.

Mwenyekiti wa Bodi anena
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Manga, Sylvester Marwa Kisiri anaushukuru mgodi huo, huku akijivunia hatua mbalimbali za maendeleo ya shule hiyo.

Kisiri anataja maendeleo mengine kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa mabweni ya wasichana na vyumba vya madarasa shuleni hapo.

“Mfano tulianza na bweni dogo lililokuwa linachukua watoto wa kike 45, lakini kwa sasa hivi yapo mengi yenye uwezo wa kuchukua watoto karibu 300,” anasema.

Kisiri ambaye ni diwani mstaafu wa kata ya Manga, anaishukuru pia Serikali Kuu kwa kuipatia shule hiyo shilingi milioni 508 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo.

Anaishukuru pia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kutenga shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi unaoendelea wa bwalo la chakula shuleni hapo.

Anaamini kwamba uboreshaji wa miundombinu hiyo pia ni chachu ya maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Shule yapaa kitaaluma
Kwa mujibu wa Mwl Nakei, maendeleo ya kitaaluma katika shule hiyo yanadhihirishwa na matokeo mazuri ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita ambayo alisema yanazidi kupanda kila mwaka.

Anafafanua kuwa wameweza kufuta alama sifuri na kuongeza ufaulu kwenye daraja la kwanza na la pili kwa miaka mitatu mfululizo.

Anasema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya watumishi (walimu na wafanyakazi wengine), lakini pia kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.

Mwl Nakei anasema walimu wamewapatia wanafunzi hao elimu itakayowajengea msingi mzuri wa kufaulu Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita na kujiunga na elimu ya vyuo vikuu na vya kati.

“Pia elimu tuliyowapatia itawajengea uwezo mzuri wa kujitambua, kufikiri na kufanya maamuzi sahihi katika kazi za ujenzi wa taifa letu,” anaongeza Mwl Nakei.

Wiki iliyopita, Mahafali ya Nane ya Wanafunzi 135 wa Kidato cha Sita yalifanyika shuleni hapo, ambapo waliahidi kufanya vizuri zaidi katika mtihani wao wa kuhitimu unaotarajiwa kufanyika Mei mwaka huu.

“Tunaahidi ufaulu wa daraja la kwanza na la pili tu katika mtihani wetu wa taifa utakaoanza Mei 6, mwaka huu. Tunaomba Mungu atupe afya njema, atulinde, atubariki na atufanikishe katika malengo yetu,” walisema wanafunzi hao kupitia risala yao kwa mgeni rasmi, iliyosomwa na Sarah Dedan na Swaumu hemed.

Shule ya Sekondari Manga kwa sasa ina wanafunzi 1,239 wa kidato cha kwanza hadi cha sita (wavulana 343 na wasichana 896), wafanyakazi wa kuajiriwa 32 wakiwemo walimu 25 na muuguzi, na walimu wa muda mfupi sita.

Hata hivyo, shule hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa nyumba za walimu, vitabu vya kiada na ziada, viti na meza, ufinyu wa chanzo cha maji na ukosefu wa mashine ya photocopy, jenereta, uzio na gari la shule, miongoni mwa mahitaji mengine.
Chanzo: SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages