NEWS

Wednesday 24 April 2024

Almasi Melau wa Arusha achambua kikokotoo cha TanzaniaWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi.
--------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
----------------------------

ALMASI Melau kutoka Ngarenaro mkoani Arusha ameandika barua ya wazi kwa wafanyakazi wa Tanzania, akichambua kikokotoo na pesheni kwa wastaafu.

Aidha, kupitia barua hiyo, Melau ameiomba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutowapunguzia wafanyakazi kikokotoo cha sasa ambacho ni miongoni mwa vikokotoo vikubwa duniani ukilinganisha na uchumi wa Tanzania.

“Naomba [Rais Samia] usitupunguzie… ukatuondolea hata hilo fao la mkupuo kama nchi nyingine na bado hawaandamani. Lakini tunaujua upendo wako kwa wafanyakazi wako wa Tanzania.

“Huko Uingereza, taifa tajiri lenye uchumi mkubwa kuliko sisi, tumesikia kikokotoo chao ni asilimia 25 tu, fedha ya mkupuo. Sisi asilimia 33 mkupuo,” amesema Melau.

Ameongeza: “Angalia wa sekta ya umma tunachangia asilimia tano tu, tunabaki na asilimia 95 zetu zote. Serikali yetu inatuchangia asilimia 15. Sekta binafsi nao wanachangia asilimia 10 na mwajiri anawachangia asilimia 10.

“Tukistaafu hatupewi mkupuo wa ile asilimia tano yetu iliyokatwa kwenye mshahara au ile 20 pamoja na ya serikali, tunapewa asilimia 33 kwa mkupuo, yaani yetu yote ile asilimia 20 na nyingine mifuko inaongeza juu asilimia 13, zaidi ya michango yetu.

“Hapo bado hatujaanza kupata pensheni, tumeshamaliza michango yetu yote tuliyokatwa na kuongezewa juu asilimia 13. Na tunaanza kupewa pensheni maisha yetu yote, hadi tunaondoka duniani. Hivi tunataka nini zaidi ya ukarimu huu?

“Huo ndio utaratibu wa pensheni duniani kote na lengo la pensheni ndilo hilo, kumtunza msafanyakazi wake asitaabike kwa kipato. Tunapewa kiinua mgongo na pensheni juu. Tushukuruni jamani,” amesema Melau.

Kwa upande mwingine, Melau ameomba elimu iliyotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) iendelee kusambazwa kwa wafanyakazi wote nchini ili kuwapa mwanga na uelewa kuhusu masuala ya kikokotoo na pensheni.

“Tanzania tunalipa mafao kijamaa zaidi. Tunatoa kiinua mgongo na pensheni kwa mpigo. Siandiki haya kuitetea Serikali au mifuko yake, bali ninataka tutende haki kama sisi tunavyotaka kutendewa haki. Lakini pia tusiingizwe mkenge na wanasiasa wakati mambo yako vizuri tu.

“Nimeona ni vizuri niwajulishe wafanyakazi wenzangu kuwa hao wanasiasa wanaotuhadaa wana malengo yao ya kisiasa. Wanatutumia tu kama chambo wakati kila kitu kiko wazi kabisa. Huku mtaani tunafuatwa na tunalishwa matango pori sana,” amesema.

Melau ametumia nafasi hiyo pia kuiomba serikali kupitia wataalamu wake kukamilisha ‘indexation’ iliyoko kwenye sheria ili wastaafu wenye pensheni ndogo sana nao wapande.

“Mwisho, ninamshukuru Rais Samia kwa kuwa msikivu na mwenye moyo wa upendo kwa wafanyakazi wenzake. Hatutaki kuifilisi nchi, ukashindwa kulipa mishahara au kutuletea madawa ya kututibu dunia ikatucheka kwa tamaa zetu,” amehitimisha Melau katika barua yake hiyo inayoonesha amepeleka nakala wa vyama vya wafanyakazi, Chama cha Waajiri Tanzania, Vyama vya Siasa Tanzania na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages