Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA Taifa, John Heche akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa chama hicho ngazi ya matawi na kata yaliyofanyika katani Sirari wilayani Tarime jana Aprili 8, 2024.
-----------------------------------------------
--------------------------------------
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ngazi ya matawi na kata wamekumbushwa kushiriki kuteua wagombea wenye sifa zinazotakiwa na wanaokubalika kwa wananchi ili kukiwezesha chama hicho kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.
Msisitizo huo ulitolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA Taifa, John Heche katani Sirari jana, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi zaidi ya 200 wa chama hicho ngazi ya matawi na kata kutoka kata tano zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijiijini.
“Tuhakikishe tunashiriki kuweka viongozi wazuri wanaokubalika kwa wananchi - watakaokuwa sauti yetu na siyo sauti ya serikali. Tujitahidi tushinde nafasi za kata, majimbo na tunahitaji kuwa na rais ili kubadilisha maisha ya watu,” alisema Heche ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini.
Awali, Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Tarime Vijijini, Tanzania Omtima katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo, alisisitiza suala la umoja na ushirikiano ndani ya chama chao kuelekea kwenye uchaguzi.
“Twendeni kama timu kwenye vitongoji na mitaa tukachukue serikali, tusidharau mtu mabadiliko ni ya msingi, tutavuka bila shida kwa kutumia mafunzo haya,” asema Omtima.
Katibu wa CHADEMA Jimbo la Tarime Vijijini, Mrimi Zabron akizungumza wakati ufunguzi wa mafunzo hayo.
------------------------------------------------
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Fatuma Abdallah Migera ambaye ni Mwenezi Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Kata ya Sirari, alisema mafunzo hayo yataongeza uelewa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mafunzo haya yanatunoa sisi kama viongozi na yanatuweka huru wanawake kiakili ili kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao,” alisema Fatuma.
Viongozi walioshiriki mafunzo hayo ni kutoka kata za Sirari, Pemba, Regicheri, Mbogi na Gwitiryo. Ratiba inaonesha kuwa mafunzo ya aina hiyo yataendelea kwa viongozi wa ngazi hizo katika kata zote 26 za jimbo la Tarime Vijijini.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka kesho.
No comments:
Post a Comment