Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------
Askari wa Jeshi la Polisi ameripotiwa kujeruhiwa vibaya na kundi la watu waliokuwa wanataka kuvamia Mgodi Dhahabu wa North Mara kwa lengo la kupora mawe yenye dhahabu jana Jumatano
“Amepigwa akazimia karibia saa sita na hali yake ni mbaya,” kimesema chanzo chetu cha uhakika kutoka eneo la tukio.
Mgodi huo unakabiliwa na tatizo la kuvamiwa na makundi ya watu wanaojulikana kama ‘intruders’ ambao wakati mwigine hukabiliana na askari polisi wanaokuwa kwenye doria katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli, na askari aliyejeruhiwa ni wa kiume,” Kamanda Njera ameiambia Mara Online News leo Alhamisi bila kutaja jina la askari huyo.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alitembelea mgodi huo na kutoa wito kwa makundi ya vijana kuacha mara moja vitendo vya kuvamia mgodi huo.
Kanali Mtambi alisema haipendezi kuona makundi ya watu yanavamia mgodi huo yakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga na mawe.
Hivyo aliwasihi watu hao kuipatia serikali nafasi ya kutafuta kile alichokiita 'sustainable solutions'.
Alidokeza kuwa tayari serikali imeweka mipango ya muda mfupi na mrefu kumaliza tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment