NEWS

Wednesday 8 May 2024

FZS yakutanisha wadau wa uhifadhi kutathmini matokeo ya mradi wa kudhibiti wanyama waharibifu na wakali



Meneja Mradi wa Shirika la Frankfurt Zoological Society - Serengeti, Masegeri Rurai akisisitiza jambo katika warsha ya kutathmini matokeo ya mradi wa kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori wilayani Serengeti mapema leo Jumatano Mei 8, 2024. Wa kwanza kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Mariko na viongozi wengine. (Picha na Mara Online News)
--------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
----------------------------------------


Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) limekutanisha wadau wa uhifadhi, viongozi wa vijiji na kata kutoka vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi, kutathmini maendeleo ya mradi wake unaolenga kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Warsha hiyo ya siku mbili imeanza leo Jumatano katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mjini Mugumu, ambapo imefunguliwa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Angelina Mariko kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya (DC), Dkt Vincent Mashinji.

“Tupo hapa leo kushirikishana matokeo ya mradi ambao umefanyika kwa takribani miaka mitatu, na kwa kufanya hivi tunasaidia Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukabiliana na wanyama waharibifu na wakali,” Meneja Mradi wa FZS Serengeti, Masegeri Rurai amewambia washiriki wa warsha hiyo.

Masegeri amesema jitihada hizo ni muhimu katika kupunguza, au kumaliza tatizo la wanyama waharibifu kama vile tembo na wanyama wakali kama simba katika vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi.

“Sio vizuri wananchi waone wanyamapori kama ni adui wao, na uhifadhi unasaidia maendeleo katika sekta ya utalii na maendeleo ya wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa mradi huo ambao pia umesaidia kuanzisha mpango wa matumzi ya ardhi katika vijiji 22 vya wilaya hiyo, unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW.


Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo.
------------------------------------------------

“Mradi huu pia umeijengea jamii katika vijiji vivyonapakana na hifadhi uwezo wa kutumia mikakati yao kuzuia wanyama waharibifu na wakali,” ameongeza Masegeri.

Kwa upande wake DAS Serengeti, Angelina amelishukuru Shirika la FZS kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa uhifadhi na shughuli za maendeleo ya wananchi katika wilaya hiyo.

Amesema juhudi za shirika hilo zinaunga mkono kwa vitendo mkakati wa kitaifa wa mwaka 2024 katika kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori nchini Tanzania.

“Wilaya ya Serengeti inaongoza kwa wanyama waharibifu, na asilimia 75 ya eneo la wilaya yetu ni eneo la uhifadhi,” amesema Angelina akionesha umuhimu wa warsha hiyo na juhudi za FZS kuendelea kuungwa mkono.

FZS ni Shirika la Uhifadhi la Kimaiafa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekumwa likisaidia Serikai ya Tanzania katika kuimarisha masuala ya uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa taribani mika 60 sasa.

Kwa miaka ya hivi karibuni, shirika hilo limekuwa likisaidia kuwezesha wananchi wanaoishi jirani na ikolojia ya Serengeti kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo ni rafiki kwa mazingira.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages