NEWS

Friday 10 May 2024

USAID, WWF wafanikisha mkutano wa wadau kujengeana uelewa kuhusu usimamizi wa pamoja wa Bonde la Mto Mara



Sehemu ya wadau walioshiriki mkutano wa kujengeana uelewa kuhusu usimamizi wa pamoja wa Bonde la Mto Mara wakiwa katika picha ya pamoja mjini Musoma jana Alhamisi wakati wa mkutano huo ulioandaliwa na WWF Tanzania kwa ufadhili wa USAID. (Picha na Mara Online News)
-------------------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Musoma
----------------------------------------------


Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania - chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), limewakutanisha wadau wa maji katika mkutano wa siku tatu wa kujengeana uelewa kuhusu usimamizi wa pamoja wa Bonde la Mto Mara kati ya nchi za Tanzania na Kenya.

Mkutano huo ambao ulihitimishwa mjini Musoma jana Alhamisi, uliwashirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji Tanzania, Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Wengine ni kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dakio la Mara, wakuu wa idara za mazingira za halmashauri za wilaya za mkoani Mara, jumuiya za watumia maji na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ambao ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa maji ya Mto Mara.


Sehemu ya washiriki wakifuatilia 
mada mkutanoni.
--------------------------------------------------

Walijadiliana na kushauriana namna nzuri ya kushirikiana na wenzao wa upande wa Kenya katika kukabiliana na shughuli za kibinadamu zinazotishia uendelevu wa mazingira hai ya Mto Mara na bonde lake kwa ujumla.

“Baada ya mkutano huu wa ndani wa kujengeana uelewa, utapangwa mkutano utakaotukutanisha na wenzetu wa upande wa Kenya kwa ajili ya kuimarisha mikakati ya usimamizi, uhifadhi na utunzaji shirikishi wa Bonde la Mto Mara,” alisema Mhandisi Lucia Lema kutoka Wizara ya Maji.

Mhandisi Emmanuel Kisendi kutoka Wizara ya Maji pia, alisisitiza kuwa suala la utunzaji endelevu wa Bonde la Mto Mara ni wa lazima, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.


Mhaidrolojia Ogoma Mangasa kutoka LVBWB Ofisi ya Mwanza akiwasilisha mada wakati wa mkutano huo.
---------------------------------------------------

Mratibu wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara unaotekelezwa na WWF Tanzania chini ya ufadhili wa USAID, Mhandisi Christian Chonya alisema bonde hilo lina mchango mkubwa kwa maisha ya binadamu na wanyama, miongoni mwa viumbe hai wengine.

Hivyo alisema mikakati ya pamoja itaimarisha nguvu ya kudhibiti vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa bonde la mto huo unaoanzia Kenya na kutiririsha maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.


Mhandisi Chonya akizungumza 
wakati wa mkutano huo.
-----------------------------------------------

Mhandisi Damas Mbaga kutoka WWF Kituo cha Bunda, alisema pamoja na mambo mengine, tayari shirika hilo chini ya ufadhili wa USAID limefanikiwa kuboresha vyanzo vya maji vipatavyo 10 katika Bonde la Mto Mara.


Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa WWF Tanzania, Joan Itanisa akizungumza katika mkutano huo.
------------------------------------------------

Mwenyekiti wa Bonde la Mto Mara Tanzania na Kenya, Sariro Mwita yeye alitumia fursa hiyo kuwapongeza WWF na USAID, akisema wamesaidia kuwajengea watu uelewa na kuwezesha shughuli za utunzaji wa mazingira ya bonde hilo. “Wamefanya kazi nzuri sana,” alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Somoche, Marko Aila alisema WWF chini ya ufadhili wa USAID wamefanikisha upandaji wa miti zaidi ya 600 kama sehemu ya kuhifadhi mazingira katika maeneo ya jumuiya hiyo.

Meneja wa Shirika la Wakulima na Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria (VIFAFIO), Majura Maingu alisema “kazi kubwa imefanyika” kwani wananchi wamehamasishwa na kuwa tayari kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ya Bonde la Mto Mara ikiwemo miradi ya ufugaji nyuki.


Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.
----------------------------------------------------

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tigite Chini, Mwita Seri alisema tayari WWF na USAID wamewapatia mizinga 25 ya kufuga nyuki na kuwasaidia uanzishaji wa kitalu cha kuotesha miche ya miti kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.

“Pamoja na mambo mengine, uhifadhi wa mazingira ndio msingi mkubwa katika uendelevu wa bonde hili,” alisema Victor Rutonesha, Afisa Maliasili na Hifadhi ya Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Wataalamu waliowasilisha mada zinazohusu uhifadhi na utunzaji wa Bonde la Mto Mara ni Dakawa Msoleni kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Gerald Itimbula kutoka LVBWB Ofisi ya Mwanza na John Ngawambala kutoka LVBWB Ofisi ya Musoma, miongoni mwa wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages