NEWS

Tuesday 28 May 2024

Barrick North Mara waadhimisha Siku ya Hedhi Duniani kwa kupeleka tabasamu kwa wasichana Sekondari ya Genge
Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------


Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara leo Jumanne wameadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani kwa kupeleka msaada wa taulo za kike na elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Genge katika wilayani Tarime, mkoani Mara.

Wakizungumza katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, wanafunzi hao wameushukuru mgodi huo wakisema taulo hizo zitawasaidia kuondokana na adha ya kutumia vitambaa wakati wa hedhi.

“Awali, tulikuwa tunatumia vitambaa lakini tunashukuru siku hizi tunapokea taulo kutoka mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kujisitiri tunapoingia katika siku zetu za hedhi,” amesema mwanafunzi Irene Samwel wa kidato cha tatu.

Mwanafunzi mwingine wa kidato hicho, Josia Chacha amesema elimu ya afya ya uzazi iliyotolewa imemwezesha kujua kuwa suala la usafi ni muhimu kwa wasichana na wanawake wakati wote, hususan kipindi cha hedhi.

“Nimejifunza kwamba mwanadamu, hasa sisi wasichana na wanawake kwa ujumla tunatakiwa kuwa wasafi muda wote na kutumia maji tiririka wakati wa hedhi ili kuondokana na maambukizi ya magonjwa,” amesema Josia.


Sehemu ya wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Genge wakifurahia msaada wa taulo za kike uliotokewa na mgodi wa Barrick North Mara.
-----------------------------------------------------

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Genge, Mwalimu Waryoba Nicholaus ameushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kutoa taulo za kike na kuandaa mpango wa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi shuleni hapo.

Aidha, Mwalimu Waryoba ametumia nafasi hiyo kutoa wito wa kuhamasisha wazazi kuvunja usiri juu ya masuala afya ya uzazi na hedhi salama kwa mabinti zao.

"Kwa mazingira yaliyopo katika jamii juu ya elimu ya afya ya uzazi kwa mtoto pamoja na hedhi salama, kuna haja ya wazazi kuvunja ukimya na kuzungumza na watoto wao," amesema.

Mwalimu huyo amesema usiri wa masuala hayo una madhara mengi kwa wasichana, ikiwa ni pamoja na kuchangia utoro wao shuleni.

Ameongeza kuwa suala la taulo za kike kwa wasichana linapaswa kupewa kipaumbele, hivyo hoja ya umaskini isiwe kigezo cha kutopanga bajeti ya kuwanunulia taulo hizo.


Afisa Maendeleo ya Jamii wa Idara ya Mahusiano Barrick North Mara, Safarani Msuya akikaribisha wanafunzi Sekondari Genge kupokea taulo za kike.
--------------------------------------------------

Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Beatrice Komba amewataka watoto wa kike kutoonea aibu suala la hedhi salama, bali waliseme kwa ujasiri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Makuri ameuomba mgodi wa Barrick North Mara kuichimbia shule hiyo kisima cha maji ili iwawie wanafunzi wa kike urahisi wa kupata maji ya kutumia wakati wa hedhi.

Mpango wa kugawa taulo za kike na elimu ya afya ya uzazi wa mgodi wa Barrick North Mara unashirikisha shule 10 katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.

Mgodi huo upo Nyamongo wilayani Tarime, na unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages