NEWS

Tuesday 28 May 2024

Mashirika ya MUJATA, Tuwakomboe yatua Nyakunguru kusaka suluhisho la uvamizi mgodi wa North Mara



Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamichele, Waitara Marara akizungumza akifungua mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mashirika ya MUJATA na TPO kitongojini hapo juzi.
--------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------


MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali ya Muungano wa Jamii za Tanzania (MUJATA) na Tuwakomboe Paralegal (TPO) yamekutana na kufanya mazungumzo na wakazi wa kitongoji cha Nyamichele katika kijiji cha Nyakunguru wilayani Tarime, kupata uelewa wa pamoja utakaosaidia kumaliza tatizo la uvamizi kwenye Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Mkutano huo ulifanyika kitongojini humo juzi, ambapo wananchi walipata nafasi ya kueleza malalamiko na maoni yao, kabla ya viongozi wa TPO, MUJATA na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuwaelimisha masuala ya utawala bora na haki za binadamu.


Sehemu ya wakazi wa kitongoji cha Nyamichele wakiwa katika mkutano huo.
--------------------------------------------

Wananchi hao walitoa mapendekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka vijana wao kupewa ajira zisizohitaji ujuzi katika mgodi wa North Mara, badala ya nafasi hizo kuelekezwa kwa watu wanaotoka maeneo ya mbali.

Pia walipendekeza kumwagiwa nje ya mgodi magwangala ya mawe (west materials) na kulipwa fidia stahiki za maeneo ya makazi yao ili wahame kutoka jirani na mgodi huo.

“Haya mambo yakitekelezwa yanaweza kusaidia kumaliza uvamizi mgodini,” alisema mmoja wa wakazi hao wa kitongoji cha Nyamichele.


Mkazi wa kitongoji cha Nyamichele akito maoni katika mkutano huo.
-----------------------------------------------

Mkurugenzi Mtendaji wa TPO Wilaya ya Tarime, Bonny Matto aliwashauri wananchi hao kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kuainisha vipaumbele vyao vya huduma za kijamii na miradi ya kujikwamua kiuchumi.

"Ninyi ndiyo mnapaswa kuanza kutengeneza bajeti kwa kufuata vipaumbele vyenu. Jengeni utamaduni wa kuhiriki kwenye mikutano na vikao mnapoitwa na viongozi wenu," alisema Matto.

Aidha, Matto aliwakumbusha kutambua kuwa ardhi ni mali ya serikali chini ya Rais kwa mujibu wa sheria za nchi, na kwamba wananchi ni wapangaji tu.


Bonny Matto akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
----------------------------------------------------

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Anthony Nyange aliwahamasisha vijana na akina mama kuunda vikundi, kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi na kuiombea ufadhili wa mitaji kutoka Halmashauri na mgodi wa North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Akina mama na vijana undeni vikundi, Mama Samia [Rais Samia Suluhu Hassan] ana fedha nyingi, kuanzia mwezi wa saba tutaanza kuzitoa, pia pesa ya CSR mkijipanga ipo kwa ajili ya miradi ya wanavikundi walio tayari," alisema Nyange.


Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamichele, Waitara Marara aliwataka wananchi na askari polisi kuheshimiana wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.

"Wananchi waheshimu polisi maana wanatekeleza majukumu yao, na polisi waheshimu wananchi. Polisi wanapokuwa wanafukuza intruders (wavamizi) wasipige mabomu kwenye makazi ya watu maana yanaathiri akina mama na watoto.

"Vijana watafute shughuli nyingine sio kwenda kushambulia polisi wakitekeleza majukumu yao, na askari wanapopita wakitekeleza majukumu yao tusiwapigie yowe," alisema Marara.

Shirika la Tuwakomboe Paralegal (TPO) lenye makao yake wilayani Tarime linajishughulisha na masuala ya sheria na utetezi wa haki za binadamu, huku Shirika la MUJATA likijikita kwenye kampeni dhidi ya maovu na kutatua migogoro katika jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages