NEWS

Friday 24 May 2024

Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara yapata wajumbe wapya



Mwenyekiti mpya wa Bodi ya WAMACU Ltd, Momanyi Range (kushoto) akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime leo Ijumaa.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News, Tarime
------------------------------------


Momanyi Range amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd), akichukua nafasi ya David Hechei aliyemaliza muda wake.

Emmanuel Ndege yeye amechaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime leo Ijumaa.



Wajumbe wa mkutano huo pia wamewachagua Kulwa Nyamhanga, Yohana Marwa na Itumbo Marwa kuwa Wajumbe wa Bodi, na James Marwa kuwa Mwakilishi wa Wakulima katika Bodi hiyo.

Viongozi na wajumbe hao watatumikia nafasi hizo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

Baada ya kuchaguliwa, wamekula kiapo cha uadilifu mbele Wakili wa Serikali na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara, Joram Kuboja.

Akizungumza katika mkutano huo, Tatu Mgenda kutoka Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika Makao Makuu Dodoma, amewakumbusha waliochaguliwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu wakitambua kuwa uongozi ni dhamana.

“Uongozi ni dhamana na aliyekuchagua anakuamini, hivyo wateteeni wakulima kwa kufuata sheria, na muwe tayari kupokea ushauri kwani uongozi pia ni sehemu ya kujifunza,” amesema Tatu.

Naye Momanyi akizungumza kabla ya kuahirisha mkutano huo, amewashukuru wajumbe na kuwaomba ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu ya kukijenga chama hicho na kuwainua wakulima.


Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya WAMACU Ltd katika picha ya pamoja baada ya uchaguzi huo.
-----------------------------------------------

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mara, Lucas Kiondere na Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, miongoni mwa viongozi wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages