NEWS

Tuesday 14 May 2024

Bomu baridi la kufukuza tembo waharibifu lavumbuliwa Tanzania
Na Mwandishi Wetu
---------------------------


Shirika la Mzinga linalomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) wamevumbua bomu baridi kwa ajili ya kufukuza tembo kwenye maeneo ya watu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bomu hilo jijini Dodoma jana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Stergomena Lawrence Tax alizipongeza taasisi hizo zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu huo, ikiwa ni matokeo ya utafiti wa kutatua tatizo la wanyama wakali na waharibifu.

Aidha, Waziri Tax aliliagiza Shirika la Mzinga kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbili ili kuja na namna bora ya kulipua bomu hilo ambalo kwa sasa linarushwa kwa mkono.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula alisema: “Tunashukuru Shirika la Mzinga kuridhia ombi la wizara kupitia TAWIRI la kuboresha vifaa vya kufukuzia tembo.”

Kitandula alisema uvumbuzi wa bomu baridi ni mafanikio makubwa kwa taifa katika kukabiliana na migongano kati ya binadamu na tembo, na ni wakati wa kuweka mikakati ya kulinufaisha taifa kiuchumi kwa kuiuza teknolojia hiyo nje ya nchi, kwani tatizo la tembo waharibifu lipo kwenye nchi nyingi za bara la Afrika.

Alibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye idadi kubwa ya wanyamapori, na asilimia 80 ya utalii unategemea wanyamapori hao. Ambapo utalii unachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt Eblate Ernest Mjingo alilishukuru Shirika la Mzinga la JWTZ Kwa kuridhia na kuboresha zana za kuondoa tembo kwenye maeneo ya watu ambapo kwa mujibu wa tafiti, baadhi ya zana zilipunguza ufanisi kutokana na tembo kuzizoea kwa kuwa ni mnyamapori wa tatu kuwa na akili nyingi.

"Bomu hili baridi ni matunda ya sayansi ambapo kwa mujibu wa utafiti, ilionekana matumizi ya vifaa vyenye sauti za mshindo mkubwa (vilipuzi) ndio kimbilio rahisi na lenye uhakika kuondoa tembo kwenye maeneo ya watu," alisema Dkt Mjingo.

Alisema vilipuzi vilivyokuwa vikitumika vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa na pia kukosekana kwa mfumo rasmi wa namna ya kuvinunua na kudhibiti matumizi yake hasa kwa ngazi za vijiji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages