NEWS

Monday 20 May 2024

Dkt Mwita Mkami awakumbusha UVCCM kujipanga uchaguzi wa serikali za mitaa



Dkt Mwita Sospeter Mkami 
akizungumza kikaoni.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
------------------------------------------


Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Dkt Mwita Sospeter Mkami amewakumbusha wanachama wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, usije ukasema tutashinda bila wewe kutumia haki yako ya kujiandikisha kwenye daftari na kupiga kura,” alisema Dkt Mkami katika kikao cha kawaida cha UVCCM Kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo jana Jumapili.

Dkt Mkami ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, alisema ushindi wa CCM kwenye chaguzi unategemea ushiriki mkubwa wa vijana kwani “uhai wa chama ni vijana”.

Sambamba na hilo, aliwataka kuunda vikundi kwenye matawi yao vya kuhamasisha wananchi wasio wana-CCM kujiunga na chama hicho tawala ili kukiongezea nguvu kwenye chaguzi zijazo.

Aidha, Dkt Mkami aliwakumbusha wana-UVCCM kuhakikisha wanachagua watu wenye sifa za uongozi kwa maendeleo ya chama hicho na wananchi kwa ujumla.

“Hakikisheni mnamchagua mtu ambaye mnaamini yuko tayari kuwatumikia, mzalendo, mwadilifu na ambaye mkimtuma anawajibika. Msimchagua mtu ambaye akiwa kiongozi anapandisha mabega,” alisisitiza.



Kwa upande mwingine, aliwahimiza kuendeleza utaratibu wa vikao na dhana ya kujitolea kwa hali na mali, ili kukijenga na kukiwezesha chama hicho kudumisha uhai wake.

“Lakini pia tukubali kokosolewa na kukosoa kwa staha, tukifaya hivyo tutaweza kusonga mbele zaidi kwa sababu kupitia kukosoana ndio tunajifunza na kuleta maendeleo ndani ya chama,” aliongeza Dkt Mwita.

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha wana-UVCCM kuwa mstari wa mbele katika kutangaza kwa wananchi kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Jitokezeni kifua mbele kusema mazuri aliyoyafanya Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake. Baada ya serikali za mitaa, uchaguzi mkuu hatuna mwingine zaidi ya Dkt Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza Dkt Mkami.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages