NEWS

Tuesday 7 May 2024

Halmashauri Tarime Mji yagawa vishikwambi kwa madiwani, DC Surumbu azindua Programu ya Malezi ya Watoto
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu (kulia) akikabidhi kishikwambi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote leo Jumanne.
---------------------------------------

Na Godfrey Marwa/
Mara Online News
------------------------------

Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara imegawa vishikwambi 11 kwa madiwani wake, vitakavyowarahisishia shughuli za upokeaji, utumaji na utunzaji wa taarifa za serikali, badala ya kutumia makabrasha.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu amewakabidhi vishikwambi hivyo wakati wa kikao chao cha uwasilishaji taarifa za kata cha robo ya tatu (Januari - Machi) ya mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo leo Jumanne.

“Hongereni sana, ukiwa kwenye biashara zako, shambani, kwenye gari utaiona taarifa kwenye kishikwambi, hakutakuwa na ucheleweshaji wa kupata taarifa, kitakuwa na nyaraka za serikali, vitunzeni visije kuibwa,” amesema DC Surumbu.

Aidha, kiongozi huyo wa wilaya ametumia fursa hiyo pia kuzindua Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) 2021/22 - 2025/26, yenye lengo la kutoa huduma za afya, lishe, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama kwa mtoto mwenye umri kuanzia sifuri hadi miaka minane.


Madiwani kikaoni
--------------------------

“Namwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tarime Mji kupitia idara zake zote zinazoratibu programu hii kuisimamia kuanzia ngazi ya halmashauri, kata na mtaa na kutekelezwa kwa mujibu wa muongozo wake.

“Wadau wa asasi zisizo za kiserikali kufuata sheria, kanuni na taratibu kwenye utekelezaji wa afua za watoto, hasa wanaoguswa na programu hii - wamiliki wote wa vituo na makao ya kulelea watoto wadogo.

“Vyombo ulinzi vya usalama vichukue hatua kwa wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na haki itendeke kwa watakaobainika - kwa ushirikiano wa wadau na idara husika,” ameagiza DC Surumbu.

Akizungumzia vishikwambi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa watavitunza vizuri na kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa.

“Hizi ni nyara za serikali, tunakuhakikishia kuvitunza kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, tulibuni kuwa na vishikwambi na hilo limetimia na tumekuwa wa kwanza kimkoa kufanya kazi kwa kutumia vishikwambi,” amesema Komote ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages