NEWS

Tuesday 7 May 2024

Huduma za upasuaji, wanawake kujifungua watoto kituo cha afya Tarime Vijijini zakabiliwa na vikwazo



Sehemu ya majengo ya Kituo cha Afya Genkuru.
----------------------------------------------

Na Mara Online News
-------------------------------


Huduma za upasuaji na wanawake kujifungua watoto zinadaiwa kukwama nyakati za usiku katika Kituo cha Afya Genkuru kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kutokana na ukosefu wa umeme.

“Kituo hiki pia hakina huduma ya maji, lakini shida kubwa zaidi ni umeme maana huduma za upasuaji na uzalishaji akina mama nyakati za usiku ni changamoto,” Diwani wa Kata ya Nyarukoba kilipo kituo hicho, Juma Matiko ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo Jumanne.

Machi 18, 2024, Mbunge Livingstone Lusinde wa Jimbo la Mtera mkoani Dodoma, na Mwita Waitara wa Jimbo la Tarime Vijijini walizuru kituoni hapo na kuzihimiza mamlaka husika kupeleka umeme na maji ili kuimarisha huduma za matibabu na afya kwa wananchi.

“Tunaomba umeme na maji viwahishwe visiwe vikwazo katika huduma za kituo hiki kwa wananchi,” alisema Mbunge Lusinde ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama tawala - CCM.

Wataalamu kutoka Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime waliahidi mbele ya wabunge hao kupeleka huduma hizo kituo hapo ndani ya wiki mbili.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Tarime, Masimino Swalo alisema ofisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa kituo hicho kinaunganishiwa umeme kufikia mwanzoni mwa Aprili 2024.

Kwa upande wake Mhandisi Mohamed Mtopa kutoka RUWASA alisema tayari wameshatenga shilingi milioni 997 kwa ajili ya kupeleka maji kituoni hapo, na kwamba mkandarasi husika alitarajiwa kuanza kazi hiyo kabla ya mwisho wa Machi 2024.

Hata hivyo, mpaka sasa hakuna kilichotekelezwa kwani kituo hicho kimeendelea kukosa umeme na maji, hali inayokwaza utoaji wa huduma za matibabu na afya kwa wananchi.

“Tunaomba serikali isikie kilio chetu, ituletee umeme na maji katika Kituo cha Afya Genkuru ili kuwezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa wakati,” amesisitiza Diwani Matiko kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kituo cha Afya Genkuru kilijengwa mwaka 2018 kutokana na shilingi zaidi ya bilioni moja zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata wasemaji wa TANESCO na RUWASA ili kujua kinachoendelea kukwamisha mipango ya kupeleka umeme na maji katika kituo hicho.

Hali hiyo inatokea huku serikali ikiendelea kusisitiza kuwa umeme na maji ni miongoni mwa huduma za kipaumbele kwenye taasisi zinazotoa huduma za kijamii, hasa zahanati, vituo vya afya, hospitali na shule.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages