NEWS

Thursday 16 May 2024

Madiwani Tarime DC waipatia CCM msaada wa viti 150, wakagua mradi wa ujenzi wa vibanda mjini



Mwenyekiti wa Tarime DC, Simion Kiles (mwenye miwani) akiongoza madiwani wenzake kukabidhi msaada wa viti 150 kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Marwa Daudi Ngicho (mwenye kofia) mjini Tarime jana Jumatano.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News, Tarime
------------------------------------


Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kimepokea msaada wa viti 150 kutoka kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles walikabidhi viti hivyo kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Marwa Daudi Ngicho katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za chama hicho mjini Tarime jana Jumatano.

“Tumetoa msaada huu wa viti kutokana na kazi nzuri inayofanyika ndani ya chama, na tutaendelea kutafuta namna ya kuongeza vingine ili chama kisikose viti vya kukalia tunapotembelewa na wageni,” alisema Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga kwa tiketi ya chama hicho tawala.


Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti Ngicho (pichani) aliwashukuru madiwani hao akisema msaada huo utaipunguzia ofisi yake mzigo wa kukodi viti vya kukalia kwenye mikutano.

“Tumekuwa tukikodi viti vya kukalia, viti 150 ni hatua kubwa vitasaidia kuondoa mapungufu yaliyokuwepo, hili ni jambo jema la kuigwa, tunawashukuru sana madiwani wa Tarime DC,” alisema.


Baadaye jopo hilo la madiwani liliongozwa na Mwenyekiti Ngicho kwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa vibanda vya biashara - ambavyo ni sehemu ya vitega uchumi vya CCM Wilaya ya Tarime.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages