NEWS

Tuesday 14 May 2024

Tanzania yapata sifa ya kuwa darasa la kimataifa la kujifunza utekelezaji miradi ya maji



Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza Bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
---------------------------------------


Tanzania, taifa ambalo kwa sasa linashuhudia kasi kubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi, imejipatia sifa ya kuwa darasa kwa nchi nyingine duniani kuja kujifunza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maji.

Hivi sasa Wizara ya Maji Tanzania na taasisi zilizo chini yake imejizolea sifa kwa kutambulika ndani na nje ya bara la Afrika kwa utendaji uliotukuka kutokana na usimamizi madhubuti wa miradi midogo na mikubwa ya maji ili kusogeza huduma hiyo muhimu karibu na wananchi mijini na vijijini.

Kwa kujiamini, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anataja mambo makubwa yaliyoitambulisha wizara yake kwa jumuiya ya kimataifa ni pamoja na Mpango wa Lipa kwa Matokeo (P4R) ambao umeiwezesha Tanzania kuwa mfano kati ya nchi 50, ikiwa ni programu inayoitambuliwa na taasisi kubwa ya kimataifa ya Benki ya Dunia.

Kutambulika kwa Tanzania kwenye ramani ya dunia kwa mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya maji, ni kichocheo kwa sekta nyingine kuboresha huduma zao ili kujenga Tanzania mpya yenye ustawi kwa wananchi wake.

Akiwasilisha Bungeni jijini Dodola Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 wiki iliyopita, Waziri Aweso alisema mambo mazuri kuhusu ukuaji wa sekta ya maji bado yanakuja.

Mambo hayo mapya ni pamoja na kuanza kutumika kwa teknolojia ya dira za maji za malipo kabla (pre-paid water meters) badala ya dira za kulipa baada ya matumizi (post-paid water meters) ili kuhakikisha uendelevu wa huduma ya maji vijijini na mijini.

Jambo jingine kubwa, kwa mujibu wa Waziri Aweso, ni kupatikana kwa chanzo kipya cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Hatifungani ambapo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga imekuwa ya kwanza kuzindua uuzaji wa Hatifungani ya Kijani yenye thamani ya shilingi bilioni 53.12.

Vipaumbele vya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ni pamoja na kuimarisha matumizi ya mitambo ya uchimbaji visima na mabwawa ili kufikisha maji kwenye vijiji ambavyo havina huduma hiyo pamoja na kutekeleza programu ya kuchimba visima 900 kwa maana ya kila jimbo la uchaguzi kupata visima vitano na ujenzi wa mabwawa madogo madogo.

“Wizara imeweka vipaumbele ambavyo vitazingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kufikia lengo la kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa mijini,” Waziri Aweso aliliambia Bunge.

Eneo jingine ambalo Wizara ya Maji itashughulika nalo ni kupunguza upotevu wa maji kwa kukarabati miundombinu chakavu, kudhibiti wizi, kufungua dira za maji ya jumla (bulk meters), kufunga dira za maji kwa wateja wote, kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji na kuwachukulia hatua wezi wa maji na uharibifu wa miundombinu.

“Lengo ni kupunguza kiwango cha maji yanayopotea kutoka wastani wa asilimia 35.3 hadi kufikia kiwango kinachokubalika kimataifa cha asilimia 20,” alisema waziri huyo mwenye dhamana ya maji.

Bunge laridhia bajeti ya
wizara kwa asilimia 100

Mabadiliko makubwa yanayotokea kwenye sekta ya maji yamelifurahisha Bunge la Jamhuri ya Muungano, hivyo kuridhia kwa asilimia 100 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kiasi cha shilingi 627,778,338,000 ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Waziri Awesso aliliahidi Bunge kwamba wizara yake imejipanga kuwa mfano kwa Tanzania kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuwahudumia wananchi.

Wizara ya Maji, ambayo tangu miaka ya 1970 ilikuwa eneo la malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwa sababu ya miradi iliyokwama, sasa imekuwa neema kwa wananchi baada ya kukamilika miradi mingi ya maji, kwa mujibu wa Waziri Aweso.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages