Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Kanali Evans Mtambi.
------------------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Mara Online News, Musoma
-------------------------------------
Serikali inatarajia kuanza kulipa fidia kwa wananchi wanaohamishwa kutoka eneo la Nyatwali katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi suala la malipo ya fidia kwa wananchi hao limefikia pazuri.
“Changamoto ya fidia kwa wananchi wa Nyatwali limefikia sehemu nzuri na siku sio nyingi akaunti zao zitaanza kucheka,” Kanali Mtambi alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Musoma Ijumaa iliyopita.
Kiongozi huyo alisema suala hilo ni miongoni mwa mengine kadhaa ambayo ameyafanyia kazi kwa ukaribu zaidi mara tu baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa huo.
Serikali inatwaa eneo la Nyatwali lenye ukubwa wa ekari 14,250 kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi hao.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, shilingi takriban bilioni 59 zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 4,000 walio kwenye orodha ya kuhamishwa katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amekuwa akihimiza serikali kuwalipa fidia wananchi hao ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment