Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (mwenye suti) akipokewa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedatus Maribe (katikati) kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25 wilayani Tarime jana. (Picha na Sauti ya Mara)
-------------------------------------------------
--------------------------------------------
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo wilayani Tarime, na kueleza kuridhishwa na kazi inayoendelea kwenye mradi huo.
Serikili ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 34.662 za mapato ya ndani kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 25.
“Naona mmefanya kazi nzuri sana, hii changamoto ya mvua nyingi na mafuriko muifanye kuwa fursa ya kutuwezesha kujua jiografia ya maeneo yetu ‘land profile’ ili tunapofanya ‘project’ au mikakati ya matumizi ya ardhi tuweze kuzingatia hali ilivyo,” RC Kanali Mtambi alisema mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo jana.
Kiongozi huyo alimtia moyo Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe katika usimamizi wa utekelezaji barabara hiyo, huku akimwahidi kushirikiana naye ili kuhakikisha pia ujenzi wa barabara ya Sanzete-Natta kwa kiwango cha lami nao unakamilika.
“Wewe [Mhandisi Vedastus Maribe] endelea na project yako, endelea na usimamizi ukitoka uje tuonane tuangalie barabara ya Sanzate-Natta nayo nilikuwa naitafutia hela, uje tuonane tuendelee kuichakata,” alisema Kanali Mtambi.
Aidha, alimshauri Mhandisi Maribe kuikumbusha Serikali kutoa fedha kwa wakati ili ujenzi wa barabara ya Mogabiri-Nyamongo ukamilike haraka na kwa kuzingatia kiwango kilichokusudiwa.
“Nikwambie kitu, kule kwenye ‘kapu’ wana miradi mingi sana kutokana na mvua na mafuriko, usipowakumbusha wanafanya na wale wanaowakumbusha, usipokumbusha hautapata, nchi kwa sasa ina changamoto nyingi za mvua,” alisema RC Kanali Mtambi.
Ujenzi wa barabara ya Mogabiri-Nyamongo unaotekelezwa na mkandarasi mzawa, Nyanza Road Works, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuunganisha miji ya Tarime na Mugumu, Serengeti na kurahisishia wananchi usafiri.
Barabara hiyo ikikamilika itakuwa kiungo muhimu kwa wakazi wa wilaya za Tarime na Serengeti, na itarahisisha usafirishaji na biashara za mazao ya kilimo kama ndizi, mahindi na kahawa yanayozalishwa kwa wingi wilayani Tarime.
Pia itachochea maendeleo ya sekta ya utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti na biashara ya madini katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, alisema.
Kwa mujibu wa TANROADS, mpaka sasa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo umezalisha ajira kadhaa kwa Watanzania.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment