NEWS

Thursday 2 May 2024

Tanzania na Kenya zamaliza mgogoro wa biashara ya kuku



Kuku wa nyama na mayai
----------------------------------

TANZANIA na Kenya zimefanikiwa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mauzo na bidhaa za kuku baina ya nchi hizo, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilisema katika taarifa yake Jumanne iliyopita.

Taarifa hiyo ilisema mzozo huo ulitatuliwa wakati wa mkutano wa mashauriano wa siku mbili uliofanyika makao makuu ya EAC jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania, uliomalizika Jumanne iliyopita.

Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, Rabson Wanjala kutoka Kenya ambaye alimwakilisha Balozi wa Kenya nchini Tanzania, alisema nchi zote mbili zimejitolea kukuza uhusiano wa kibiashara.

Wanjala aliongeza kuwa ahadi zao zinasisitiza juu ya umuhimu wa juhudi za ushirikiano ili kuhakikisha biashara inaongezeka katika ukanda huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Benezeth Lutege Malinda alisema Tanzania inashughulikia kikamilifu vikwazo vya kibiashara kwa kuhakikisha mashirika yote yanayowezesha biashara yanajikita katika kutatua masuala, hususan vikwazo visivyo vya ushuru vinavyokwamisha biashara.

"Tunaendelea kujitolea kukabiliana na changamoto hizi na kukuza mazingira mazuri ya biashara kati ya Kenya na Tanzania," alisema Malinda.

Mwaka 2018 Tanzania ilichoma vifaranga 5,000 vya kuku kutoka Kenye vilivyodaiwa kuingizwa nchini humo kupitia mpaka wa kaskazini wa Namanga.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages