NEWS

Friday 3 May 2024

RC Mtambi azuru mgodi wa Barrick North Mara, aonya ‘intruders’



Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (kulia) akimwonesha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati) sehemu ya eneo la mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime wakati alipozuru mgodini hapo leo Mei 3, 2024. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu. (Picha na Mara Online News)
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
----------------------------


MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi leo Mei 3, 2024 amefanya ziara ya kwanza katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na kuyataka makundi ya watu kuacha kuvamia mgodi huo ambao amesema una faida nyingi kwa jamii inayouzunguka na taifa kwa ujumla.

RC Mtambi amesema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Huu ni uwekezaji mkubwa (is one of the mega projects) na manufaa ya uwekezaji huu ni makubwa kweli, sio kwa eneo la Nyamongo tu au Tarime, bali kwa kwa nchi yetu kwa ujumla,” amesema.

Ameeleza pia kufurahishwa na uwekezaji wa mabilioni ya fedha ambao umefanywa na kampuni ya Baririck kwenye miradi ya kijamii ndani na nje ya mkoa wa Mara.

“Naona mmefanya kazi nyingi kwenye community (jamii), mabilioni ya fedha yamewekeza kwenye miradi ya maendeleo, nitoe shukrani kwa kazi nzuri mnayofanya, mboreshe zaidi,” amesema RC Mtambi.

Ameongeza: “Niweke wazi jambo ambalo si ajabu Watanzania wengi hawafahamu, mradi huu sio wa mwekezaji peke yake, Serikali ya Tanzania nayo ni mwekezaji, tuna hisa zetu.”

RC Mtambi amesema tayari Serikali imeweka mipango ya muda mfupi na mrefu kuhakikisha mwekezaji huyo anafanya kazi kwa manufaa makubwa zaidi bila bughudha za kuvamiwa na makundi ya watu wanaojulikana kwa jina la ‘intruders‘.

“Serikali ipo tayari kwa hali yoyote, niweke wazi hilo,” ameonya kiongozi huyo -akiwataka vijana kuacha kuvamia mgodi huo ili kuipatia serikali nafasi kile alichokiita 'sustainable solutions'.

Ameweka wazi kuwa hatapenda kuona nguvu ikitumika kuzuia uvamizi huo, lakini akasisitiza kuwa ikilazimu nguvu itatumika.

Amesema uvamizi ukiendelea unaweza kuchelewesha kupata masuluhisho endelevyu (sustainable solutions).

“Mnaona mgodi huu unavyojali mazingira na jamii inayouzunguka," amesema.

Ameongeza kuwa haipendezi kuona makundi yatu wanavamia mgodi huo wakiwa na siraha za jadi kama vile mapanga na wakati mwingine kukabiliana na askari wa jeshi la polisi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya, SACP Mark Njera akifafanua jambo kwa RC Mtambi.
--------------------------------------------------

Awali, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amemweleza RC Mtambi kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyokabili shughuli za mgodi huo ni uvamizi (intrusions), tegesha (land speculations) na uchimbaji haramu.

Hata hivyo, GM Lyambiko amesema mgodi huo unaendelea kufanya juhudi mbalimbali kumaliza matatizo hayo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa kushirikisha wadau wakiwemo viongozi wa kijamii.

Katika ziara hiyo, RC Mtambi pia amefuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, miongoni mwa wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages