NEWS

Monday 27 May 2024

Serikali yatoa onyo kali dhidi ya ‘intruders’ mgodi wa North Mara, yapiga marufuku siasa kwenye misiba TarimeMkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu (aliyesimama) akizungumza katika kikao chake na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) Nyamongo Alhamisi iliyopita.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------


Serikali wilayani Tarime imetoa onyo kali na kuyataka makundi ya watu wanajulikana kama ‘intruders’ kuacha mara moja vitendo vya uvamizi katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Maulid Surumbu alitoa onyo hilo Alhamisi iliyopita wakati wa kikao cha dharura kati yake na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), kilochofanyika Nyamongo ulipo mgodi huo kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

“Rasilimali iliyopo hapa Nyamongo kwa mujibu wa sheria zetu, itatumika kwa manufaa ya Watanzania wote, lakini pia kwa sheria, wananchi wanaozunguka mgodi kuna namna wanahudumiwa, na ninyi ni mashahidi na mmetoa mifano ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa.

“Mgodi kwa upande wao wana mambo ya kufanya, kwa hiyo yale ambayo yapo kimkataba twendelee kuyatekeleza, lakini uvamizi kwenye mgodi nao tunautolea maelekezo ukome mara moja,” alisisitiza Kanali Surumbu na kuendelea:

“Serikali yetu kuanzia ngazi ya kata, vijiji na vitongoji iende kusimamia agizo hili na tutoe ushirikiano, maana sehemu wanapojikusanya vijana hawana kufanya mambo haya ya kihalifu ni kwenye maeneo yetu.”

Kikao hicho kilifanyika siku moja baada ya vijana wawili kuripotiwa kupoteza maisha wakati wakikabiliana na askari polisi waliokuwa wakiwazuia kuingia ndani ya mgodi huo kupora mawe ya dhahabu.

DC Kanali Maulid alisema serikali ya wilaya itagharimia mazishi ya vijana waliopoteza maisha katika tukio hilo, huku akiliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika Kwenda kinyume na sheria za nchi.

“Polisi wafanye uchunguzi, kama kuna makosa ya kiutendaji kwa askari atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo, lakini kwa wale ambao wamevamia basi nao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Lakini na mimi naungana na mkuu wa mkoa kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopata msiba ambao umetokana na uvamizi kwenye mgodi. Serikali itagharimia gharama za msingi kwa wafiwa wote wawili,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo pia kupiga marufuku tabia ya wanasiasa wanaotumia matukio ya vifo vya wavamizi wa mgodi wa North Mara ili kujipatia umaarufu kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Misiba yote kwenye wilaya ya Tarime isitumike kama majukwaa ya siasa, hii ni kwa vyama vyote vilivyopo wilaya ya Tarime; haviruhusiwi kufanya siasa kwenye misiba, tuitishe mikutano ya hadhara tufanye siasa zetu,” alisisitiza Kanali Surumbu.

Aliongeza: “Lakini pia kwa wale wanaochochea uhasama kwa namna yoyote ile na kuwashawishi vijana kwamba mgodi ule [North Mara] ni halali yao, na leo kwenye kikao hiki tumeona kabisa vijana hawana wanachodai kwenye mgodi ule, pia waache mara moja kuwashawishi vijana hao.”

Mkuu hiyo wa wilaya alisisitiza kuwa wachochezi wa vitendo vya uvamizi kwenye mgodi huo lazima washughulikiwe kisheria.

“Yeyote anayefanya uchochezi wa aina yoyote ile kwenye misiba, au nje ya misiba atachukuliwa hatua za kisheria,” Kanali Surumbu alisema na kumwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kutochelewa kuchukua hatua dhidi ya wachochezi hao.

“OCD nataka uchukue hatua mara moja kwa yeyote ambaye atabainika kufanya mambo ya uchochezi kwenye mikutano, au kwenye misiba katika wilaya yetu ya Tarime.

“Lakini pia Afisa wa Madini wa Mkoa aje afanye ukaguzi wa krasha ambazo hazina vyanzo vya kupata mawe kwenye maeneo haya, na wale watakaobainika kwamba hawana vyanzo vya mawe, basi leseni zao zichunguzwe na ikiwezekana zifungiwe,” alisema Kanali Surumbu.

Viongozi wengine waliohudhulia kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simon Kiles, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, viongozi wa kata na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.

Baada ya kikao hicho, kiongozi huyo wa wilaya na msafara wake walikwenda kuwapa pole ndugu wa vijana waliopoteza maisha katika makabiliano na askari polisi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages