
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akikabidhi kikombe cha ushindi kwa mwakilishi wa timu husika, wakati wa kilele cha mashindano ya UMITASHUMTA Mkoa wa Mara, Juni 12, 2026. Wa kwanza kulia ni Afisa Michezo Mkoa wa Mara, Mwl. Makondo Makondo.
Tarime
-----------
Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) 2026 katika mkoa wa Mara, yamefikia kilele kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mashindano hayo ambayo yalianza Mei 20 na kuhitimishwa Juni 12, 2026, yamewezesha kupatikana kwa wanamichezo bora 120 watakaowakilisha mkoa wa Mara kwenye michuano ya ngazi ya taifa itakayofanyika mkoani Iringa.

Sehemu ya wanamichezo 120 walioteuliwa kuwakilisha mkoa wa Mara katika mashindano ya UMITASHUMTA 2026 yatakayofanyika mkoani Iringa.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwapongeza na kuwataka wanamichezo hao kuzingatia nidahamu, uvumilivu na bidii ili kuuletea mkoa wa Mara ushindi katika michezo yote.
"Niwapongezeni, juhudi zenu ndizo zimewafanya mchaguliwe, mmekabidhiwa bendera na Mkuu wa Mkoa, uteuzi uliofanyika umezingatia viwango na vigezo, mkatuwakilishe vizuri.
"Mmepewa dhamana, sio kwa upendeleo, ni kwa sababu ya uwezo wenu, tunawatakia kila la heri, mkatuletee ushindi wa mkoa mkiwa wa kwanza kwenye michezo yote,” alisema DC Gowele.

DC Gowele (aliyevaa kofia nyeusi waliosimaama), walimu na wanamichezo walioteuliwa kuwakilisha mkoa wa Mara katika mashindano ya UMITASHUMTA 2026 ngazi ya taifa. (Picha zote na Mara Online News)
Afisa Michezo Mkoa wa Mara, Mwl. Makondo Makondo, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, aliahidi ushindi mkubwa kupitia kikosi hicho cha wanamichezo.
"Tunakuahidi kurudi na ushindi mkubwa kuliko mwaka jana, ukitufungia tutaenda na baraka,” alisema Mwl. Makondo.
No comments:
Post a Comment