NEWS

Saturday 4 May 2024

Tarime Mji wazindua mashindano ya UMISETA kupata timu za kushiriki ngazi ya mkoaNa Godfrey Marwa, Tarime
-------------------------------------


HALMASHAURI ya Mji wa Tarime mkoani Mara imezindua mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) katika viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime.

Mashindano hayo yalizinduliwa juzi na Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa wa halmashauri hiyo, Mwl Teddy Musyangi ambaye alisema yatawezesha kupatikana kwa wachezaji mahiri wa michezo mbalimbali wapatao 120 watakaoiwakilisha kwenye ngazi ya mkoa.


“Mashindano yalianzia ngazi ya kata na leo [juzi] yanaanza ngazi ya kanda ili kupata timu ya Halmashauri ya UMISETA mwaka 2024 itakayokwenda kushiriki mashindano ya kimkoa yatakayofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, kisha mkoani Tabora katika ngazi ya kitaifa kwa michezo yote,” alisema Mwl Musyangi.

Alitaja michezo hiyo kuwa ni pamoja na riadha, mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu na kurusha mkuki.


Mwl Teddy Musyangi
-----------------------------


Alitoa wito kwa wazazi kuwaruhusu watoto kushiriki michezo mbalimbali ili kuibua na kukuza vipaji vyao kwa manufaa yao na taifa.

“Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan [Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania] imeelekeza kukuza vipaji vya watoto, wazazi wawaruhusu watoto hususan wa kike kuja kushiriki kwenye michezo, michezo ni ajira kama ajira zingine, sio uhuni wala kupoteza muda. Mtoto anaweza kuwa mchezaji soka, msanii wa kuimba,” alisema.

Mwl Musyangi alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuiunga mkono serikali katika ununuzi wa vifaa vya michezo kwa ajili ya wanafunzi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages