NEWS

Friday, 6 March 2026

Barrick yawezesha wanawake kushiriki mnyororo wa thamani sekta ya madini



Mgeni rasmi, Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu (wa tatu kutoka kulia mbele), akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao (Female Future Program), wakiwemo watano kutoka Barrick North Mara pamoja na viongozi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wakati wa mahafali yao jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026, kampuni ya Barrick nchini yenye ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals, imeendeleza dhamira yake ya kuhakikisha wanawake wanapewa fursa sawa katika ushiriki wa mnyororo wa sekta ya madini.

Hivyo, Barrick imewawezesha wafanyakazi wake wanawake watano kupata mafunzo ya uongozi kupitia programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao (Female Future Programme) yanayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), inayolenga kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wa kike mahali pa kazi.

Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao ambayo ilianzishwa mwaka 2015, imefikia kundi (Cohort) la 11 ikiwa inajumuisha wanawake wasomi kutoka kampuni mbalimbali, ilianzisha ATE kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri nchini Norway na katika kipindi cha muda mfupi imekuwa msaada mkubwa katika kuwajengea uwezo wa utawala katika sehemu zao za kazi.


Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hotuba mbalimbali wakati wa mahafali yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam

Akihojiwa kuhusu ushiriki katika progamu hiyo, mmoja wa wahitimu kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Edith Biita, alisema anajivunia kuajiriwa na kampuni kubwa kama Barrick ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwapatia wafanyakazi wanawake nafasi za uongozi na inayomuwezesha kutoa maamuzi ambayo yeye na wafanyakazi wenzake wanawake ndani ya kampuni wanayo fursa ya kutoa mawazo yao na yamekuwa yakiheshimiwa bila kujali jinsia na umri wao.

Akiwa ni msomi wa fani ya uhandisi wa madini akifanya kazi katika kitengo cha uchimbaji na milipuko (drill and blast), Biita alisema mafunzo aliyopata kupitia programu hiyo ni ya aina yake kwa kuwa yanawezesha kupata maarifa ya masuala mbalimbali, hususani utawala kwa kuwa katika fani zote suala la utawala na uongozi lipo.

Sella Mwaigomole, mtaalamu wa metolojia na maabara, alisema mafunzo yanayotolewa na programu hiyo yanawezesha kujiamini zaidi katika utawala na alitoa ushauri kwamba kuna haja ya kuwa na programu nyingi za aina hiyo ili ziwafikie wanawake wengi popote walipo nchini ili wasibaki nyuma katika utawala kwenye sekta mbalimbali.

“Ili wanawake wengi kutobaki nyuma silaha pekee ya kuwakwamua ni elimu na ninaposema elimu simaanishi kupata shahada za juu pekee bali ni kujifunza mambo mbalimbali na kupata maarifa, kuungana na kushirikiana, ambapo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali, kupeana moyo na kupanga mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Mwaigomole.


Wahitimu wa Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao (Female Future Program) ya ATE kutoka Barrick North Mara katika picha ya pamoja. Kuanzia kushoto ni Patricia Vulla, Elda Mahenda, Sella Mwaigomole, Edith Dickson Biita na Noela Mataro wakati wa mahafali yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Naye Noela Mataro aliishukuru Barrick kupitia mgodi wa North Mara kwa kumpatia fursa ya kupata mafunzo haya ya utawala na kuongeza kuwa anavutiwa na sera ya kampuni ya kuwapatia nafasi za uongozi wanawake katika vitengo mbalimbali, ambapo wanaendelea kufanya vizuri na kudhihirisha kuwa ujuzi hauna jinsia.

Mshiriki mwingine kutoka Barrick, Patricia Vullah, alisema mpango wa kuwapatia wanawake mafunzo ya utawala ya Female Future Programme ni moja ya jukwaa la kuwanyanyua wanawake wa Tanzania na kuwafikisha kwenye nafasi za juu za uongozi na kutoa maamuzi.

Kwa upande wake, Elda Mahenda alisema kupitia programu hiyo wanafundishwa masuala mengi, hususani utawala wenye kuleta ufanisi kwa kampuni, kujiamini na jinsi ya kushiriki na kuchangia mawazo katika vikao vya juu vya bodi za kampuni.

“Mtaala wa kufundishia unaotumika ni mzuri na ndani ya kipindi cha muda mfupi unaweza kumbadilisha mtu kuwa na maarifa, upeo mkubwa na kujiamini,” alisema.


Wahitmu hao kutoka Barrick North Mara wakiwa wamepozi kwenye picha ya pamoja

Kampuni ya Barrick nchini imekuwa mstari wa mbele kutekeleza sera imara ya kukuza usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi na kiufundi katika migodi yake ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa.

Pia, Barrick inazingatia ushirikishwaji wa wanawake, mafunzo na programu za ndani na nje zinazolenga kukuza vipaji vyao ili kuongeza uwakilishi katika ngazi za maamuzi.

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Kampuni ya Barrick inatumia siku hiyo kama jukwaa la kutathmini na kuendeleza juhudi za wanawake kazini, kusaidia jamii zinayozunguka migodi na kuchochea wanawake kuingia katika sekta ya madini ambayo awali ilitawaliwa na wanaume.

Juhudi hizo za uwezeshaji wanawake zinaendana na sera ya serikali ya kuongeza ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) na kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika mnyororo wa sekta ya madini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages