Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika
Mkoa wa Mara, Momanyi Range.
------------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Musoma
------------------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Ushirika wa mkoa huo.
Mkutano huo wenye kaulimbiu inayosema “Ushirika kwa Maendeleo Endelevu”, umepangwa kufanyika Mei 15 - 16, mwaka huu katika ukumbi wa CCM Mkoa mjini Musoma.
Akizungumza na Sauti ya Mara katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) mjini Tarime juzi, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Momanyi Range alisema mkutano huo utaangazia mafanikio na changamoto za wanachama wake.
"Lengo kuu la mkutano ni kuwakutanisha wanajukwaa wa mkoa wa Mara kwa ajili ya kuleta mafanikio yao, pamoja na changamoto zao ili tuweze kusaidia kuzitatua, lakini pia kuangalia kwamba mkulima mdogo kupitia ushirika anasaidiwa aweze kujiinua kiuchumi na kuendeleza ushirika mkoani Mara," alisema Momanyi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi za kifedha, serikali na mashirika, kwa lengo la kuwasaidia wanaushirika kukuza vipato na uchumi wao kwa ujumla.
Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara limekuwa likiunganisha wadau kutoka vyama mbalimbali vya ushirika mkoani humo, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi na sekta ya madini, miongoni mwa wengine.
No comments:
Post a Comment