NEWS

Monday 6 May 2024

Watetezi wa haki za binadamu Tanzania watembelea mgodi wa Barrick North Mara



Wawakilishi kutoka mashirika yanayotetea haki za binadamu Tanzania wakiwa katika ziara kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime juzi. Watano kutoka kushoto ni Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Taifa, Onesmo Olengurumwa na na wa pili kushoto ni Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi ambaye pia alifuatana na baadhi ya wafanyakazi wenzake.
--------------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania wamefanya ziara muhimu katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, Tarime koani Mara.

“Sisi kama watetezi wa haki za binadamu tumekuja kujifunza, kufuatilia na kujionea mambo ambayo tumekuwa tukishauri yafanyike katika mgodi huu,” Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Taifa, Onesmo Olengurumwa aliwambia waandishi wa habari wakati wa zaira hiyo Ijumaa iliyopita.

Alisema kipindi cha miaka ya nyuma ilikuwa vigumu kwa mgodi huo kuruhusu watetezi wa haki za binadamu kuutembelea na kupata fursa ya kukagua masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusu maslahi ya wafanyakazi na jamii inayouzunguka.

“Hii ni hatua nzuri maana mwisho wa siku hii ni nchi yetu na sisi tunapaswa kushiriki kushauri masuala muhimu ili kulijenga taifa hili la Tanzania,” alisema Olengurumwa.

Alisema ziara hiyo iliwapatia fursa ya kuangalia namna mgodi huo unatekeleza sera mbalimbali.

“Tunaangalia namna wanafanyia kazi sera mbalimbali, mfano kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, wafanyakazi na suala la ujirani mwema,” alifafanua.

Mgodi huo unaendeshewa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, watetezi hao wa haki za binadamu walipata fursa ya kuzuru katika maeneo mbalimbali ya mgodi huo, likiwemo bwawa la majitaka (TSF) na kituo kikubwa cha kuzalisha na kutibu maji (water treatment plant).

Olengurumwa alisema kuna umuhimu wa kampuni au mashirika mengine kuiga mfano huo wa Kampuni ya Barrick ili waweze kupata fursa ya kuwatembelea na kuona namna wanavyozigatia haki za binadamu katika shughuli zao.

Mashirika zaidi ya 10 wanachama wa THRDC yalishiriki katika ziara hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal (TPO) linalofanya shughuli zake wilayani Tarime, Bonny Matto alisema mgodi huo umeendelea kufanya vizuri katika kuzingatia masuala ya haki za binadamu, hivyo kupunguza malalamiko kutoka kwa jamii inayouzunguka ulikingaisha na miaka ya nyuma.

Matto alitoa mfano akisema: “Miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko na migogoro ya maji machafu, tumepita hatua kwa hatua wanaonesha jinsi walivyopiga hatua kuzuia maji machafu yasiende popote na wanayafanyia ‘Recycling’, sasa maji hayo yanatumika, hata mimi ndiyo nimeoga na kunawa, ni hatua nzuri sana.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages