NEWS

Thursday 16 May 2024

Waumini wafungiwa na kuteketezwa Msikitini Kaskazini mwa Nigeria


Wakazi wanaoshi karibu na Msikiti ulioteketezwa kwa moto Jimboni Kano Kaskazini mwa Nigeria wakijaribu kuuzima moto huo
------------------------------------------


Waumini wasiopungua 11 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mtu mmoja jana jioni kushambulia msikiti katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria.
 
Polisi wanasema mtu mmoja anadaiwa kuunyunyizia msikiti petroli na kufunga milango ya Msikiti huo kabla ya kuuteketeza kwa moto, ndani wakiwemo waumini takriban 40
Shambulio lilichochewa na mgogoro wa familia juu ya mgawanyo wa urithi.

Polisi wanasema wamemkamata mtuhumiwa mwenye umri wa miaka 38.

Tukio hilo lilitokea watu walipokuwa wakihudhuria sala za asubuhi siku ya Jumatano katika eneo la Gezawa jimboni Kano. Wakaazi walisema moto uliozuka uliteketeza msikiti baada ya shambulio huku washirika wakisikika wakiomboleza wakati walipokuwa wakijaribu kufungua milango iliyofungwa.


Sehemu ya mabaki ya Msikiti ulioteketezwa kwa moto katika Jimbo La Kano Kaskazini mwa Nigeria
--------------------------------------------


Polisi baadaye walisema bomu halikutumiwa katika shambulio hilo. Huduma ya zimamoto ya Kano ilisema hawakuitwa mara moja baada ya moto kuanza, wakiongeza kuwa wangeweza kudhibiti hali hiyo haraka zaidi. Msemaji wa Huduma ya zimamoto ya Kano, Saminu Yusuf, aliiambia BBC kuwa walikuwa wamearifiwa baada ya wenyeji kuzima moto tayari.

"Katika hali kama hii, watu wanapaswa kutuita lakini hatukupata simu yoyote kutoka eneo hilo hadi baada ya hali ya kawaida kurudi," Bw Yusuf aliongeza.

Polisi walisema mtuhumiwa alikiri kwamba vitendo vyake vilikuwa sehemu ya mzozo juu ya urithi, akidai alikuwa anawalenga baadhi ya wanafamilia waliokuwa ndani ya msikiti huo.

"Kilichotokea hakihusiani na kitendo chochote cha ugaidi, badala yake ilikuwa ni mzozo uliojitokeza kama matokeo ya ugawaji wa urithi," Umar Sanda, afisa wa polisi wa eneo hilo, aliiambia waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la tukio. "Mtuhumiwa yupo nasi kwa sasa na anatoa taarifa muhimu," Bw Sanda aliongeza.

Ripoti za awali zilisema mmoja wa washirika alikuwa amekufa kutokana na shambulio lakini idadi ya vifo iliongezeka baadaye baada ya wahanga zaidi kufa wakati wakipokea matibabu katika Hospitali Maalum ya Murtala Muhammad huko Kano.

Sheikh Dauda Sulaiman anasema kuua watu wakati wanaposali ni moja ya dhambi kubwa zaidi  na kwamba mbali na kutubu kwa Mungu, mkosaji anapaswa kulipa fidia kwa familia za wale waliokufa. Kijiji kizima sasa kipo katika maombolezo. 
 
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages