NEWS

Friday 21 June 2024

‘AICT, Right to Play waungwe mkono uhamasishaji haki sawa kwa watoto’Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyantira wilayani Tarime, Peter Patrobe akikabidhi jezi kwa wanafunzi wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa ushirikiano na Right to Play katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyantira jana.
-----------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime
------------------------------------


Jamii imehimizwa kuzingatia uhamasishaji wa haki sawa kwa watoto wote, ikiwemo ya elimu bora kwa mtoto wa kike, unaotolewa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyantira wilayani Tarime, Peter Patrobe alisisitiza hayo kwenye tamasha la michezo ya wanafunzi lililoandaliwa na taasisi hizo katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyantira jana, ili kuelimisha jamii umuhimu wa kuwapa watoto wote haki sawa.

“Wazazi na walezi tuweke mkazo wa kuwapeleka watoto wetu shule hasa hawa wa kike, tuepuka kuwatendea ukatili kama vile ukeketaji maana wana changamoto nyingi, hivyo tuwasaidie kupambana nazo na tuhakikishe wanapata elimu bora kama AICT na Right to Play wanavyohimiza,” alisema Patrobe.

Naye Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisema taasisi hizo zinashirikiana kuelimisha jamii umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, pamoja na kuwasaidia kukabiliana na vikwazo vya masomo.

Daniel Fungo akizungumza katika tamasha hilo.
-----------------------------------------------

"Vikwazo wanavyokutana navyo watoto wa kike katika elimu ni pamoja na ukeketaji, ndoa za utotoni na vipigo vya mara kwa mara, hivyo sisi tunashirikiana kuihamasisha jamii itambue umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, lakini pia kusaidia kuondoa vikwazo hivyo,” alisema Fungo.

Kwa upande wake Neema John Marwa ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Nyantira, aliwashukuru AICT na Right to Play kwa kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu, na kupungua kwa vitendo vya ukatili dhidi yao.

Tamasha hilo la michezo lililohusisha pia wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Muringi, ni mwendelezo wa maadhimisho ya kumbukizi ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 kila mwaka, kuwakumbuka watoto waliopoteza maisha huko Soweto nchini Afrika Kusini katika harakati za kudai haki zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages