NEWS

Friday 21 June 2024

Halmashauri Tarime Mji yapata hati safi miaka minne mfululizo, RC Mara aipongezaMkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (wa tatu kushoto) akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime jana.
----------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
------------------------------------


Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kupata hati safi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesbu za Serikali (CAG) kwa miaka minne mfululizo.

“Halmashauri hii imepata hati safi kwa miaka minne mfululizo, Baraza lako [Mwenyekiti] limefanikiwa kuimarisha Kamati ya Ukaguzi kwa mujibu wa sheria na linaendeshwa kidijitali kwa kutumia vishikwambi, hongereeni, nawapongezeni sana kwa hilo,” alisema RC Mtambi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo jana.

Hata hivyo, alilitaka Baraza la Madiwani kuendelea kusimamia menejimenti ya halmashauri hiyo ili kuhakikisha inaendelea kupata hati safi miaka ijayo.

Madiwani kikaoni
--------------------------

Aidha, RC Mtambi aliielekeza halmashauri hiyo kuhakikisha inajibu na kutekeleza kwa wakati hoja zote za Mkaguzi wa Ndani, kuzingatia taratibu za ununuzi wa umma, kuelekeza mapato ya ndani kwenye ukamilishaji wa miradi viporo na kushirikisha wananchi katika uibuaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Pia Mkurugenzi ahakikishe madiwani na watendaji wanapata mafumzo kuhusu sheria ya ununuzi wa umma na kanuni zake, baraza lisimamie mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,” aliongeza RC Mtambi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao aliahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages