NEWS

Sunday 30 June 2024

Bob Wangwe atembelea Ofisi za Gazeti la Sauti ya Mara, ahimiza weledi kwenye habari za siasa na chaguzi



Mtia nia ya ubunge katika jimbo la Tarime Mjini, Bob Wangwe (Chadema), akifafanua jambo wakati alipotembelea ofisi za Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, na kufanya mazungumzo na Mhariri Mtendaji wa vyombo hivyo vya habari, Mugini Jacob (kulia), leo mchana.
----------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------

Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Bob Wangwe amevipongeza vyombo vya habari vya Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara kwa kazi nzuri vinayoifanya ya kuhabarisha jamii.

Bob ambaye pia ni mtia nia ya ubunge katika jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ametoa pongezi hizo alipotembelea ofisi za vyombo hivyo vya habari, mjini Tarime leo mchana.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, endeleeni kuibua changamoto za wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi,” Bob amewambia Wahariri wa vyombo hivyo, Mugini Jacob na Christopher Gamaina.

Kuhusu habari za siasa na uchaguzi, amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma, ikiwemo kutoa habari bila kuegemea upande wowote.

Mhariri Mtendaji Mugini Jacob (kulia), akimkabidhi Bob Wangwe (mwenye miwani) na rafiki zake nakala ya Gazeti la Sauti ya Mara.
---------------------------------------------

Kwa upande mwingine, Bob amempongeza Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara, Mugini Jacob kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC).

“Kuchaguliwa kwako kuwa Mwenyekiti wa MRPC kumeonesha jinsi unavyoaminiwa na waandishi wa habari wa mkoa wa Mara,” Bob amemwambia Jacob.

Bob Wangwe ni mtoto wa Chacha Zakayo Wangwe aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kwa tiketi ya Chadema, kati ya mwaka 2005 na 2008, kabla ya kufariki dunia kutokana na ajali ya gari.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages