NEWS

Monday 1 July 2024

Uongozi: Kiles anavyoendelea kuifungua kata ya Nyakonga kimaendeleoDiwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles akizuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kijijini Magoto wiki iliyopita.
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU
----------------------------------

Wananchi wa kata ya Nyakonga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara, wana kila sababu ya kujivunia maendeleo ya kisekta wanayopata chini ya uongozi wa Diwani wao, Simion Kiles.

Tangu achaguliwe mwaka 2020, Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, amekuwa mpambanaji hodari wa maendeleo ya wananchi wa kata ya Nyakonga.

Mfano, kati ya mwaka 2020 na 2024, kata hiyo chini ya uongozi wake imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya huduma za kijamii yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni mbili, zikiwemo kutoka serikalini, mfuko binafsi wa diwani huyo na michango ya wananchi.

Wiki iliyopita, viongozi wa vijiji vya Nyakonga, Magoto na Kebweye vinavyounda kata ya Nyakonga walimwalika Diwani Kiles kwenye mikutano ya hadhara ya kusomea wananchi wao taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Miradi iliyotekelezwa

Katika mkutano wa kijijini Magoto, Afisa Mtendaji wa Kijiji, Sinda Ryoba alisema wamefanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni moja katika kipindi hicho cha miaka minne.

Ryoba alitaja miradi iliyotekelezwa kutokana na fedha hizo kuwa ni pamoja na ya elimu, afya, maji na barabara.

“Tunamshukuru diwani wetu, umetutua ndoo yam aji kichwani akina mama wa Magoto, hata kwenye huduma za afya zamani tulilazimika kwenda kuzitafuta kijijini Nyarero, lakini siku hizi wao ndio wanakuja hapa,” alisema Lucy Range katika mkutano huo wa kijijini Magoto.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyakonga, Petronila Chiriko akisoma taarifa ya maendeleo ya kijiji hicho, alisema wao wameweza kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu, maji, barabara na umeme yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 548 kati ya mwaka 2020 na 2024.

Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kebweye, Charles Chacha Nchagwa alisema shilingi zaidi ya milioni 969 zimetumika kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini hapo katika kijiji hicho.

Diwani Kiles (katikati mwenye miwani) akipokewa na wananchi kijijini Nyakonga.
-------------------------------------------

Awashukuru wananchi
Akizungumza kwa siku na nyakati tofauti katika mikutano hiyo, Diwani Kiles aliwashukuru wananchi wa vijijini hivyo na kata ya Nyakonga kwa ujumla, kwa ushirikiano mzuri wanaouonesha kwake na viongozi wengine katika juhudi za kuwaletea maendeleo.

Aidha, Kiles aliwakumbusha wenyeviti wa vitongoji na vijiji katani humo kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kusikiliza, kupokea na kutafuta utatuzi wa kero za wananchi wao.

Hata hivyo, diwani huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji hadi ngazi ya halmashauri kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo na kuwaletea maendeleo ya kisekta.

Alisema hatua hiyo itahusisha kufuatilia na kuhakikisha kuwa miradi yote viporo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika kata ya Nyakonga inakamilishwa.

“Kila kijiji nitaweka alama, nahitaji nije nikumbukwe na vizazi kwa vitu vinavyoonekana,” alisema Diwani Kiles.

Alisema kwa sasa tayari shilingi milioni 506 zimetengwa na Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo, shilingi milioni 280 zimetengwa katika bajeti ijayo kwa ajili ya jengo la mama na mtoto la kituo cha afya Magoto na shilingi milioni 50 za ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti kituoni hapo.
Sehemu ya wananchi wakifuatilia mazungumzo ya Diwani wao wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles katika mkutano wa hadhara kijijini Magoto.
-----------------------------------------------

Kwa upande mwingine, Kiles alivikumbusha vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu kukaa mkao wa kula kwani Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iko mbioni kuanza kuvipatia mikopo ya fedha isiyo na riba kwa ajili ya kuendesha miradi ya kujikwamua kiuchumi.

“Kwenye pesa za asilimia kumi halmashauri tumekusanya bilioni 9.1, zinasubiri maelekezo ya Rais, hivyo jiandaeni kuweka vikundi vizuri na muwe tayari kupokea mikopo kwa ajili ya kufanyia miradi itakayowakomboa kiuchumi na kijamii,” alisema.
Kuwasaidia wazee

Katika hatua nyingine, Diwani Kiles aliahidi ‘kuwapiga jeki’ wazee wa katani Nyakonga watakaoungana na kuanzisha mradi wa kilimo biashara.

“Wazee unganeni mkodishe mashamba, nitawashika mkono, nitawasaidia mbolea na mbegu ili nanyi muweze kujikwamua kiuchumi,” alisema Kiles.

Diwani huyo aliendelea kusisitiza kuwa maendeleo ya kata ya Nyakonga yataletwa na mshikamano wa wananchi wake wanaochapa kazi na kuwapuuza watu wenye nia ya kuwagawa.

“Hii kata iliongozwa na upinzani kwa miaka 15, tulikuwa kisiwani, hatukuwa na mawasiliano kwenda vijiji vya Kebweye na Nyarero. Watu walikimbia hiki Kijiji cha Nyakonga kwa sababu ya michango, ila kwa sasa kazi inaendelea na inaonekana, hivyo wapuuzeni na tusiwape nafasi wenye nia ya kutuchonganisha,” alisema.
Amshukuru Rais Samia

Kiles alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiidhinishia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, wakiwemo wa Nyakonga.

Hivyo aliwaomba wananchi hao kuendelea kukiamini chama tawala - CCM, akisema ndicho chenye uwezo wa kutatua changamoto zao na kuwaletea maendeleo.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages