NEWS

Thursday 6 June 2024

Chandi, Gachuma wateta na madiwani wote wa CCM mkoani Mara
Na Mwandishi Wetu, Mara
------------------------------------


Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara umekutana na madiwani wote wanaotokana na chama hicho mkoani humo kuweka mikakati ya ushindi katika uchaguzi wa viongozi serikali za mitaa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Kikao hicho kilifanyika wilayani Tarime jana, ambapo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Christopher Mwita Gachuma na Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Ibrahim Mjanakheri walizungumza na madiwani hao na kuwapa maelekezo mbalimbali yanayolenga kukihakikishia chama hicho ushindi wa kishindo katika chaguzi hizo.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa akizungumza na madiwani hao katika kikao hicho.
----------------------------------------------------

“Ninyi ndio mpo karibu na wananchi, diwani akishinda, mbunge atashinda na Rais atashinda pia kwa kishindo,” alisema MNEC Gachuma katika sehemu ya hotuba yake kwa madiwani hao.

Pia aliwataka kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha ambayo imetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Nimekuwa kwenye system (mfumo) muda mredu, sijawahi kuona kipindi cha neema ambacho fedha nyingi za maendeleo zimemwaga kwenye maeneo yetu kama kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Dkt Samia,” alisema Gachuma.


MNEC Gachuma akizungumza 
na madiwani hao.
--------------------------------------------------

MNEC huyo alisema Rais Samia anastahili kupewa miaka mitano tena kutokana na kazi nzuri anayofanya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kisekta. “Mama Samia ni mtu mpole na ana faida nyingi sana,” alisema.

Kikao hicho kilifunguliwa na kufungwa na Chandi ambaye anatajwa kuwa Mwenyekiti bora wa CCM katika mkoa wa Mara alikozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa upande wao madiwani hao walisema kikao hicho kimekuwa cha manufaa makubwa kwao.

“Kwa kweli viongozi wetu wametueleza mambo mengi muhimu na mazuri, na wametutia moyo sana,” alisema Farida Joel ambaye diwani mwanamke wa kata ya Kenyamanyori katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages