NEWS

Thursday 27 June 2024

Diwani awapa wazee wa kata ya Nyakonga wazo la kujikwamua kiuchumiWakazi wa kijiji cha Nyakonga akifuatilia jambo mkutanoni jana Jumatano.
------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
-------------------------------------

Diwani wa Kata ya Nyakonga katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, Simion Kiles ameahidi ‘kuwapiga jeki’ wazee wa katani humo watakaoungana na kuanzisha mradi wa kilimo biashara.

“Wazee unganeni mkodishe mashamba, nitawashika mkono, nitawasaidia mbolea na mbegu ili nanyi muweze kujikwamua kiuchumi,” alisema Diwani Kiles wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Nyakonga jana Jumatano.

Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya utoaji wa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wanakijiji tangu mwaka 2020 hadi 2024.

Simion Kiles akihutubia mkutano huo.
------------------------------------------------

Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), alitumia nafasi hiyo pia kuvikumbusha vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu kukaa mkao wa kula kwani halmashauri hiyo iko mbioni kuanza kuvipatia mikopo ya fedha isiyo na riba kwa ajili ya kuendesha miradi ya kujikwamua kiuchumi.

“Kwenye pesa za asilimia kumi halmashauri tumekusanya bilioni 9.1, zinasubiri maelekezo ya Rais, hivyo jiandaeni kuweka vikundi vizuri na muwe tayari kupokea mikopo kwa ajili ya kufanyia miradi itakayowakomboa kiuchumi na kijamii,” alisema.

Diwani huyo alisema maendeleo ya kata ya Nyakonga yataletwa na mshikamano wa wananchi wake wanaochapa kazi na kuwapuuza watu wenye nia ya kuwagawa.

“Hii kata iliongozwa na upinzani kwa miaka 15, tulikuwa kisiwani, hatukuwa na mawasiliano kwenda vijiji vya Kebweye na Nyarero. Watu walikimbia hiki Kijiji cha Nyakonga kwa sababu ya michango, ila kwa sasa kazi inaendelea na inaonekana, hivyo wapuuzeni na tusiwape nafasi wenye nia ya kutuchonganisha,” alisema Kiles.

Awali, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyakonga, Petronila Chiriko (pichani) akisoma taarifa ya maendeleo ya kijiji hicho, alisema shilingi zaidi ya milioni 548 zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya, barabara, shule, maji na umeme kati ya mwaka 2020 na 2024.

Nao wanakijiji walipewa nafasi ya kueleza kero zao, zikiwemo za kucheleweshewa nguzo za umeme katika baadhi ya vitongoji, kuchafuka kwa maji ya bwawa wanayotumia na huduma zisizo rafiki katika kituo cha afya katani Nyakonga, ambapo Diwani Kiles aliahidi kuzifikisha kwenye mamlaka husika kwa hatua za ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages