NEWS

Monday 10 June 2024

Kutana na ‘intruder’ wa mgodi wa North Mara aliyeamua kupiga teke uhalifu huoKijana Emmanuel Daniel Magebo akichangia mada kwenye mdahalo wa fursa za uwekezaji uliofanyika mjini Tarime hivi karibuni.
-------------------------------------------------

Na Christopher Gamaina
---------------------------------


Inawezekana kabisa. Ndivyo tunavyoweza kuelezea uamuzi ya kijana Emmanuel Daniel Magebo aliyekuwa akijishughulisha na vitendo vya uvamizi katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Kijana huyu ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyakunguru kilichopo jirani na mgodi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, sasa ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na jinsi alivyobadilisha historia ya maisha yake.

Uamuzi wake wa kuachana na vitendo vya uvamizi na wizi wa mawe ya dhahabu mgodini, umekuwa chachu ya maendeleo yake ya kujijenga kiuchumi.

Tofauti na enzi zake za uvamizi mgodini, kwa sasa kijana huyu ni mmiliki wa nyumba ya kudumu na miradi ya kilimo na biashara ndogo ndogo - inayompatia kipato cha kuendesha maisha na familia yake ya wake wawili na watoto wanane.

“Nimekuwa intruder (mvamizi) mgodini tangu mwaka 2009 hadi 2013 (miaka minne) nilipoamua kuacha uhalifu huo. Pesa nyingi niliyopata kwa wakati mmoja nikiwa intruder ni shilingi milioni 15, nikanunua pikipiki moja, zilizobaki nilitumia zikaisha ndani ya muda mfupi, kisha nikauza pikipiki nikatumia zikaisha.

“Kimsingi nilipokuwa intruder sikuweza kumiliki kitu chochote cha maana, lakini sasa hivi ninamshukuru Mungu ninamiliki vitu vya maana.

“Kwanza nimejenga nyumba ya kuduma ya makazi, na nina miradi ya shamba, biashara ya bodaboda (pikipiki ya kubeba abiria) na duka la vifaa vya pikipiki kijijini kwetu,” alisema kijana Magebo katika mahojiano na Sauti ya Mara mjini Tarime, wiki iliyopita.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba Magebo pia ameajiri watu wanaomsaidia kuendesha baadhi ya miradi hiyo. “Nimeajiri vijana wawili shambani na mmoja kwenye bodaboda,” anafafanua.

Ajira yake nyingine
Zaidi ya hayo, kwa sasa Magebo pia ni mwanachama wa kutunukiwa na mmoja wa vijana sita walioajiriwa katika kikundi kilichoanzishwa na wanawake kinachojulikana kwa jina la Utu Group kilichopo kijijini Nyakunguru.

Yeye ni dereva wa gari la kikundi hicho ambacho kinajishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya mgodi wa North Mara.

“Nilipoacha uvamizi mgodini nilitafuta kazi ya ulinzi, kisha nikajiongeza nikaenda kusoma udereva wa magari ambao umeniwezesha kupata ajira kwenye kikundi hiki cha Utu,” anasema Magebo.

Anaweka wazi kuwa shughuli hizo zote zimemwezesha kubadilisha hali ya maisha yake kutoka kwenye umaskini wa kipato na uvamizi wa mgodi hadi kufikia hatua ya kuwa na uchumi wa kati.

Utu Group walivyomsaidia
Mwenyekiti wa Utu Group, Nyangi Mwita Waitara anasema yeye na wenzake ndio walimshauri na kumshawishi Magebo kuachana na vitendo vya uhalifu mgodini ili kujiunga na kikundi hicho.

“Tulimshawishi Magebo kuachana na uvamizi mgodini baada ya kuona vitendo hivyo vina madhara kwa vijana,” anasema Nyangi.

Anabainisha kuwa hadi sasa kikundi hicho kimeajiri vijana sita wa kiume waliokuwa wakijihusisha na uvamizi na wizi wa mawe ya dhahabu kwenye mgodi wa North Mara.

“Kati ya hawa vijana sita, wawili akiwemo Magebo tuliwashawishi kuacha wizi mgodini ili wajiunge na kikundi chetu, na wanne waliamua wenyewe kuacha vitendo hivyo na kuja kuomba kuungana nasi baada ya kuona hao wawili wanapiga hatua ya maendeleo,” anafafanua.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Utu Group, mmoja wa vijana sita waliowaajiri ni mhitimu wa chuo kikuu na watano ni wahitimu wa kidato cha nne.

“Mwanzoni walipojiunga na kikundi chetu walikuwa wakirudi siku moja moja mgodini kwa kificho lakini tulipogundua tuliwakemea hadi wakaacha kabisa vitendo hivyo.

“Mfano huyu mwenye digrii (mhitimu wa chuo kikuu) tulimuonya tukamwambia ukiendelea kwenda kufanya uhalifu mgodini utakufa na elimu yako hata kabla haujaoa, basi hatimaye wote wakaacha kabisa, na sasa hivi kila mmoja amepiga hatua nzuri kimaendeleo,” anasema Nyangi.

Wito kwa vijana wengine
Hivyo basi, kijana Magebo na Mwenyekiti huyo wa Utu Group wanatumia nafasi hiyo pia kutuma wito na ushauri kwa vijana wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya uvamizi na wizi wa mawe ya dhahabu katika ngodi wa North Mara kuachana na uhalifu huo na kutafuta njia halali za kujipatia kipato.

“Nashauri vijana wenzangu, hasa wavamizi wa mgodi kutafuta namna nyingine ya kujipatia kipato, ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata fursa za kufanya biashara na mgodi, lakini pia kupata mikopo kutoka Halmashauri yetu ya Wilaya.

“Kwenda mine [akimaanisha kuvamia mgodi] hakusaidii kwa sababu ni kujiweka kwenye hatari ikiwemo ya kupoteza maisha. Kwa hiyo, kupitia vikundi, vijana wanaweza kupata fursa nyingine, ikiwa ni pamoja na kujiajiri kwenye kilimo wakawa wakulima na wakaajiri watu wengine,” anasema Magebo.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages