NEWS

Monday 3 June 2024

Tarime Mji waadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani 2024, wapeleka furaha kwa wagonjwa na wafanyakazi boraBaadhi ya wauguzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime wakiwa katika picha ya pamoja juzi.
-------------------------------------------------

Na Timothy Itembe, Tarime
-------------------------------------


Idara ya Afya katika Halmashauri ya Mji wa Tarime imeadhimisha Siku Wauguzi Duniani mwaka huu wa 2024 kwa kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi bora na kuwafariji wagonjwa.

“Wengi wetu wanajituma na kufanya kazi vizuri na leo tumeona tuwazawadie baadhi yetu ambao wanajituma kazini,” Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Joshphine Aloyce Ninga alisema katika sherehe iliyofanyika Hoteli ya Blue Sky juzi jioni.

Wafanyakazi waliozawadiwa ni kutoka hospitali hiyo na baadhi ya zahanati na vituo vya afya, vikiwemo vya Magena na Mugini Polyclinic kilichopo mjini Tarime.


Mmoja wauguzi bora, Nassoro Abdallah Yakub akipokea zawadi katika hafla ya Siku ya Wauguzi Duniani 2024 iliyoandaliwa na Idara ya Afya katika Halmashauri ya Mji wa Tarime juzi. (Picha na Sauti ya Mara)
------------------------------------------------------

Wauguizi hao walitumia fursa hiyo pia kuaga baadhi ya wauguzi wenzao waliostaafu na kuwapa zawadi mbalimbali.

Mgeni Rasmi katika sherehe hiyo alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki ambaye aliwakilishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Marema Sollo.

Kembaki aliahidi kuwachangia wauguzi hao shilingi milioni tano ili waweze kuanzisha mradi wa kitega uchumi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji wa Tarime, Dkt Elias Makima aliwapongeza wauguzi hao kwa kuendelea kujituma na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt Makima pia aliwashukuru wadau wote waliosaidia kufanikisha hafla hiyo.

Awali, wauguzi hao wa Tarime Mji walitoa wito wa kuwakumbisha wauguzi wote duniani kufanya kazi kwa moyo wa upendo, huku wakizingatia miongozo yao ya kitaaluma, ikiwemo kuwatunzia wagonjwa siri.

“Siku yetu wauguzi tunamkumbuka mwanzilishi wetu wa huduma ya uuguzi, Florence Nightingale. Mama huyu alifanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa kwa upendo sana.

“Kwa hivyo na sisi kama wauguzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime tunaienzi siku yake hii ya kuanzisha huduma hii ya uuguzi.

“Lakini pia ndiyo siku ambayo tunarudia kiapo chetu cha kutukumbusha kwamba sisi ni wauguzi na tunastahili kufanya kazi kulingana na miongozo yetu," alisema Josephine.


Muuguzi Joshphine akigawa biskuti 
kwa watoto hospitalini hapo.
----------------------------------------------

“Pia katika siku hii tulikuwa na zawadi kidogo, tumeshirikisha upendo huu kwa zawadi kwa wagonjwa wetu, tumetoa sabuni za kufulia kwa akina mama wanaojifungua katika wodi ya wazazi na biskuti zenye sukari kwa watoto ili kuwaongezea nguvu.

“Wauguzi wote duniani tufanye kazi kwa moyo na upendo, lakini pia tuzingatie miongozo yetu ya kazi, na kikubwa hasa ni kufanya kazi kwa moyo na kuwatunzia siri wagonjwa wetu.

“Jamii ninaisihi ituelewe sisi ni wauguzi kama zilivyo kada nyingine na sisi ni watu ambao tumeenda shule tukajifunza kuwahudumia, watuelewe tuko kwa ajili yao na serikali inatulipa na kutuwezesha katika stahiki zetu katika kutoa huduma hii,” alisema Josephine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages