NEWS

Tuesday 25 June 2024

Waathirika wa wanyamapori waharibifu na wakali walalamikia "vifuta jasho duni", Tarime Vijijini wadai hawajawahi kulipwa kwa miaka zaidi ya 50Tembo

NA CHRISTOPHER GAMAINA, Mara
--------------------------------------------------

Wananchi mkoani Mara wameeleza kutoridhishwa na kile ambacho wanadai ni malipo duni ya vifuta jasho na machozi, wakitaka sheria iliyopo ifanyiwe marekebisho kuboresha viwango vya malipo hayo kwa wananchi wanaoathiriwa na wanyamapori.

Vinginevyo, wamesema serikali itarajie kushuhudia ongezeko kubwa la umaskini uliokithiri kwa wananchi ambao mifugo na mashamba yao vinashambuliwa na wanyamapori waharibifu na wakali wakiwemo tembo, chui na fisi.

Mara ni moja ya mikoa ya Tanzania bara ambayo wananchi wake wanapakana na maeneo ya mbuga za wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mapori ya Akiba ya Ikorongo- Grumeti.

Wakizungumza na Gazeti la Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti hivi karibuni, baadhi ya madiwani kutoka wilaya za Serengeti na Tarime walisema viwango vya malipo vinavyotolewa kufidia mifugo na mashamba vilivyoathiriwa na wanyamapori ni vidogo kwani haviakisi hali halisi ya maisha ya sasa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kifuta Jasho/ Machozi ya Mwaka 2011, viwango vinavyotolewa na serikali kufidia mifugo iliyouawa na wanyamapori ni shilingi 50,000 kwa ng’ombe mmoja, 25,000 kwa mbuzi, au kondoo mmoja.

Aidha, kulingana na sheria hiyo, malipo ya vifuta machozi kwa ndugu wa mtu aliyeuawa na wanyamapori ni shilingi milioni moja, na kwa aliyejeruhiwa ni shilingi laki tano.

Kwa upande wa mashamba ya mazao yaliyoharibiwa, fidia ni kati ya shilingi 25,000 na 100,000 kwa ekari moja kutegemeana na umbali uliopo kati ya shamba husika na hifadhi ya wanyamapori.

“Hivyo viwango ni vidogo sana, haviendani na uhalisia wa maisha ya sasa, hakuna mbuzi anayeuzwa shilingi 25,000, hakuna ng’ombe anayeuzwa shilingi 50,000 hata kama ni ndama,” alisema Diwani wa Kata ya Nagusi wilayani Serengeti, Andrew Mapinduzi katika mazungumzo na Sauti ya Mara kwa njia ya simu.

“Bei ya mifugo siku hizi imepanda katika masoko yote duniani, ni kuanzia shilingi laki moja kwa mbuzi au kondoo, na laki tano hadi milioni moja kwa ng’ombe,” aliongeza diwani huyo kutoka chama tawala - CCM.

Fisi

Kuhusu mashamba, Mapinduzi alisema fidia ya shilingi laki moja kwa ekari moja iliyoharibiwa haifikii hata nusu ya gharama zilizotumika kulima na kupanda mazao.

“Katika dunia ya sasa hivyo viwango vya malipo ya vifuta jasho ni vidogo. Chukulia mtu analima ekari moja kwa shilingi 50,000 halafu ananunua mbegu kwa shilingi 60,000, bado gharama ya mbolea, kulipa watu wa kupanda na kupalilia, halafu unakuja unamlipa laki moja.

“Hivi viwango havikubaliki, watu wanaumia na wana hali mbaya kiuchumi. Hiyo sheria inayotumika imepitwa na wakati, tunataka ifanyiwe marekebisho kuongeza viwango vya malipo ya vifuta jasho ili kumpunguzia mwananchi madhara aliyopata.

“Yawezekana hiyo sheria iliyopo iliwekwa wakati mbuzi anauzwa shilingi 2,000 hadi 3,000 lakini kwa sasa huwezi kupata mbuzi kwa shilingi 25,000, hakuna,” alisema Mapinduzi.

Hata hivyo, wananchi wanalalamika kwamba mara nyingi viwango hivyo havitolewi kwa wakati. “Kuna watu huku katani kwangu wana miaka zaidi ya mitatu hadi minne hawajalipwa vifuta jasho vyao,” alisema diwani huyo.

Naye Diwani wa Kata ya Nyambureti, Peter Bachuta pia kutoka wilayani Serengeti, ambaye hivi karibuni kondoo wake 14 waliuawa na fisi, aliomba serikali kutopuuza kilio cha wananchi wanaotaka viwango vya malipo ya vifuta jasho vipandishwe.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kwihancha wilayani Tarime, Ragita Ragita alisema hata hivyo viwango duni vya vifuta jasho havijawahi kulipwa kwa wananchi wa katani kwake.

“Waathirika wa wanyamapori wamejaa hapa katani kwangu, tangu mwaka 1974 vijiji vilivyoanza hakuna mwananchi wangu aliyewahi kulipwa. Ni mwaka huu tu kama miezi mitatu hivi iliyopita tumeona maofisa wa halmashauri ya wilaya wameleta fomu za vifuta jasho na machozi vikajazwa na waathirika.

“Msimu huu mashamba mengi yemeharibiwa na tembo katani kwangu. Watu wameletewa fomu wamejaza, tunasubiri tuone lakini hatuna imani kabisa, maana mimi kama kiongozi nimeshapigia kelele tatizo hilo serikalini kwa miaka mingi lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Kinachonishangaza ni jinsi ambavyo serikali yetu imeshindwa kusimamia sheria ilizotunga ili waathirika walipwe hata kwa hivyo viwango vidogo vya vifuta jasho na machozi,” alisema Diwani Ragita pia kutoka chama tawala - CCM.

Chui

Miezi michache iliyopita, chui alivamia nyumbani kwa mkazi wa kijiji cha Robanda wilayani Serengeti, Mechakobo Ketenana na kuua mbuzi na kondoo 34.

Afisa Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan alizungumza na Sauti ya Mara kuhusiana na tukio hilo na kuthibitisha kuwa malipo ya fidia kwa mbuzi au kondoo mmoja aliyeuwa na mnyamapori ni shilingi 25,000 kulingana na kanuni zilizopo.

Kwa hesabu hiyo, Ketenana alitarajiwa  kulipwa shiingi 850,000 kama kifuta jasho kutokana na mifugo yake 34 [mbuzi na kondoo] iliyouawa na chui nyumbani kwake kijijini Robanda.

Robanda ni miongoni mwa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti na mapori ya akiba ya Ikrongo-Grumeti katika ikolojia ya Serengeti mkoani Mara.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages