NEWS

Tuesday 25 June 2024

Serikali yatenga shilingi zaidi ya bilioni moja kuchangia ujenzi wa sekondari mbili Musoma Vijijini



Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, 
Profesa Sospeter Muhongo.
---------------------------------------------


NA MWANDISHI WETU, Musoma
-----------------------------------------------

Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga shilingi 1,168,560,000 kuchangia ujenzi wa shule mbili za sekondari katika jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo wiki iliyopita, ilibainisha kuwa shule hizo zitajengwa katika kata za Nyamrandirira na Bukima.

“Kwenye kata ya Nyamrandirira shule mpya ya sekondari itajengwa katika kijiji cha Kasoma, na kwenye kata ya Bukima sekondari mpya itajengwa kijijini Butata,” taarifa hiyo ilifafanua.

Ujenzi wa kila shule umetengewa shilingi milioni 584.28, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Rai ya Mbunge
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo ameshauri viongozi wa serikali na chama wa kata, vijiji na vitongoji wahamasishe wananchi kuchangia nguvu kazi ili miundombinu mingi ya elimu ipatikane kutokana na fedha hizo.

“Pia tunashauri maeneo ya ujenzi yasiwe na migogoro, wananchi wafuatilie matumizi ya fedha za ujenzi kwa karibu na ujenzi ukamilike mapema ili ifikapo Januari 2025, sekondari hizo mpya zifunguliwe,” alisema Prof Muhongo.

Maombi mapya
Kwa upande mwingine, Mbunge huyo amepokea na kukubali maombi ya ujenzi wa shule mpya za sekondari katika vijiji vya Kataryo kilichopo kata ya Tegeruka, Kiriba (Kiriba) na Mmahare (Etaro).

“Mbunge wa jimbo ameyakubali maombi hayo na baada ya vikao vya Bunge vinavyoendelea ataenda kuongoza harambee za kuanza ujenzi wa sekondari hizo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ilisema vijiji vingine zaidi ya vitano vimeomba kujenga sekondari mpya lakini mipango yao haijakamilika.

Sekondari zinazojengwa
Shule za sekondari zinazojengwa kwa nguvu za wananchi na viongozi wao katika jimbo la Musoma Vijijini kwa sasa ni Rukuba (Kisiwa) katika kata ya Etaro, Nyasaungu (Ifulifu), Kurwaki (Mugango) na Muhoji (Bugwema).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ofisi ya Mbunge, tayari serikali imeanza kuchangia ujenzi wa shule hizo kwa kutoa shilingi milioni 75.

Hadi sasa kuna shule za sekondari 28 zinazofanya kazi katika jimbo la Musoma Vijijini lenye kata 21 na vijiji 68.

Kati ya hizo sekondari 28, 26 ni za kata/serikali na mbili ni za binafsi.

Lengo la jimbo
Lengo kuu la jimbo la Musoma Vijijini ni kila kata kuwa na sekondari mbili, au zaidi. Mfano kata ya Nyamrandirira yenye vijiji vitano ifikapo Januari 2025 itakuwa na sekondari tatu katika vijiji vya Kaboni, Seka na Kasoma.

“Wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini tunaendelea kuishukuru serikali yetu chini ya uongozi mzuri wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za miradi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, na uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwenye shule zetu,” ilihitimisha taarifa hiyo.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages