NEWS

Tuesday 25 June 2024

RC Mara ameona mbali utekelezaji miradi ya CSR Barrick Tarime Vijijini



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (wa pili kushoto) akitoa maelekezo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilayaya Tarime, Ijumaa iliyopita. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya, Kanali Maulid Surumbu. Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji, Solomoni Shati (wa nne kushoto).
------------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU
--------------------------------

Ijumaa iliyopita, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) kufanya makubaliano na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa shilingi bilioni tisa.

Fedha hizo zimetengwa kwa mara nyingine na mgodi huo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomoni Shati, utekelezaji wa mpango wa CSR Barrick North Mara kwa sehemu kubwa utajikita kwenye miradi ya kijamii, ambayo ni vipaumbele vya wananchi wa maeneo husika, kama vilivyowasilishwa na wawakilishi wao, yaani madiwani.

Ikumbukwe kuwa madiwani wa halmashauri hiyo ndio wamepanga miradi itakayotekelezwa na kupitisha bajeti yake miezi michache iliyopita.

Katika kikao cha madiwani hao kilichofanyika katani Nyamwaga Ijumaa iliyopita, RC Mtambi aliielekeza halmashauri hiyo kukutana na kufanya makubaliano na mgodi huo ndani ya wiki hii, ili utekelezaji wa miradi husika uanze haraka.

Sambamba na hilo, aliielekeza halmashauri hiyo kuhakikisha inabeba jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kupitia kwa wataalamu wake, na sio mgodi wa Barrick North Mara ambao umekwishatekeleza wajibu wake wa kutoa fedha za CSR.

Matarajio ya wengi ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Tarime itatekeleza maelekezo haya ya Mkuu wa Mkoa, hasa ukizingatia kuwa madiwani wake ndio walioainisha miradi ya CSR na kupitisha bajeti yake.

Naam, Halmashauri inastahili kubeba jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa sababu ina wataalamu walioajiriwa na serikali kwa ajili hiyo.

Na ikumbukwe kuwa mwaka jana Kampuni ya Barrick iliipatia halmashauri hiyo gari jipya kwa ajili ya shughuli za kufuatilia na kusimamia miradi ya CSR.

Kwa upande mwingine, madiwani nao wana jukumu la kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ya CSR Barrick, sambamba na kuitangaza kwa wananchi ili wajue faida za uwekezaji katika mgodi wa North Mara.

Tunataka hatua zote za usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi husika zilenge kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa na mgodi huo hazitumiki vibaya, kama vile kunufaisha watu binafsi - kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Wananchi na mwekezaji [Barrick Gold] aliyetoa fedha hizo za CSR, wanatarajia kuona na kusikia miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyoakisi thamani ya fedha iliyotumika (value for money), si vinginevyo.

Mambo yote haya ni muhimu kuzingatiwa na kila mhusika kwa sababu lengo la utekelezaji wa miradi hiyo ya CSR Barrick, ni kuwapunguzia wananchi kero na kuwaletea maendeleo, ikiwemo kuwaboreshea huduma za kijamii.

Tunatarajia pia utekelezaji wa miradi hiyo utakuwa chachu ya kuwabadilisha watu wenye mitazamo hasi dhidi ya mgodi wa Barrick North Mara, wakiwemo wanaojihusisha na uhalifu wa kuuvamia, kuiba mawe ya dhahabu na kuharibu miundombinu yake.

Mungu bariki utekelezaji wa miradi ya CSR Barrick North Mara, ibariki Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) na wananchi wake.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages