Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia) akisikiliza maelezo kwenye banda la maonesho ya madini wakati alipokwenda kufunga maadhimisho ya Wiki ya Madini jijini Dodoma leo.
--------------------------------------------------
-----------------------------------------
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya nchi kutafuta teknolojia za kuongeza thamani madini.
Amesema kufanya hivyo kutawezesha madini yanayopatikana nchini kutumika kuzalisha bidhaa ambazo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka duniani.
Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Madini iliyoambatana na Kongamano la Wachimbaji Madini, Mkutano Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) na Maonesho ya Madini na Vifaa vya Uchimbaji, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo Juni 27, 2024.
Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara, taasisi za elimu na fedha, Wizara za Madini, Viwanda na Biashara kuendelea kuweka mikakati ya kuwezesha uwekezaji wa ndani wa teknolojia mbalimbali zitakazowezesha upatikanaji wa malighafi zinazohitajika kwenye migodi na shughuli nyingine za madini.
“Kwa kuwa teknolojia duniani inazidi kukua kwa kasi, wadau wa madini waongeze na kuimarisha mtandao na wachimbaji wa kikanda na kimataifa. Kujifungia ndani peke yetu hatutapata suluhisho la changamoto tulizonazo, bali tutachelewesha maendeleo yetu,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Majaliwa amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto, kero na adha zinazowakabili wawekezaji na wachimbaji wa madini, pamoja na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika ya kuuza madini, lakini pia kuendelea kuwezesha wawekezaji wadogo katika sekta ya madini kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha nchini ili waweze kupewa mikopo.
“Katika hili nitoe wito kwa taasisi za fedha nchini kukaa na FEMATA, wapeni miongozo na elimu ya mitaji waweze kuitumia katika kuzipa thamani kazi zao ili ziwe na tija,” amesema.
Kwa Upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa nguvu sekta ya madini ili iendelee kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231.
“Mipango yetu ni kuendelea kufanya tafiti za kina ili kubaini sehemu yalipo madini, pia tumepanga kununua helkopta ya kisasa ya itakayobaini kilichopo hadi urefu wa kilomita moja chini ya ardhi, pamoja na kujenga maabara kubwa ya kisasa katika sekta ya madini,” amesema.
Ameongeza kuwa wizara hiyo inaendelea kutekeleza mpango wa kufuta leseni na maombi kwa wawekezaji waliochukua maeneo makubwa ya uchimbaji madini lakini hawayaendelezi, ili iweze kuwapatia Watanzania wenye nia ya kuchimba wanufaike na rasilimali hiyo muhimu.
Naye Rais wa FEMATA, John Wambura amesema Tanzania ina fursa ya kuwa na soko la madini Afika kwani ina kila sifa ya kufikia hapo, na hiyo ni kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia.
Wambura amesema kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025, FEMATA imepanga kuendelea kuwaomgezea ujuzi na maarifa wachimbaji wadogo wengi zaidi, sambamba na kuwaunganisha na serikali ili kusaidia kuongeza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.
“Pia tumeandaa vitambulisho ili tuweze kutambua kila mchimbaji alipo na anafanya nini,” ameongeza Wambura.
No comments:
Post a Comment