NEWS

Friday 28 June 2024

DAS ataja zawadi, faida za Tamasha la Nyama Choma TarimeKatibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari ((hawapo pichani) alipokutana nao ofisini kwake leo mchana kuzungumzia Tamasha la Nyama Choma.
----------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------

Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara imeendelea kuwaalika wananchi wote kuhudhuria na kushiriki Tamasha la Kuchoma Nyama, huku ikitaja zawadi kwa washindi na faida za tamasha hilo litakalofanyika Julai 3, mwaka huu.

“Tamasha hilo litahusisha mashindano ya kuchoma nyama za ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku,” amesema Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Mwalimu Saul Mwaisenye, katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake leo mchana.

Kuhusu zawadi, DAS Mwaisenye ambaye amezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu, amesema mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi 500,000, wa pili (300,000) na wa tatu (200,000).

Amebainisha kuwa tamasha hilo ambalo kwa lugha ya kigeni limeitwa Tarime Nyama Choma Festival, litafanyika katika eneo la mnada wa Mtana uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni.

“Kuanzia saa nne asubuhi nyama choma laini, tamu na bora zitakuwa zinatafunika pamoja na kichuri pale mnadani, huku zikisindikizwa na muziki nyororo,” amesema DAS Mwaisenye na kuongeza:

“Lakini pia, kama tunavyojua nyama choma zinaendana na vinywaji kama vile soda na bia, hivyo wafanyabiashara wa vinywaji nao wanakaribishwa kwa ajili ya ku- support mashindano ya kuchoma nyama.”

Kwa mujibu wa DAS Mwaisenye, tayari Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeshakutana na wafanyabiashara ya nyama choma, na kuwahamasisha kuchangamkia fursa hiyo ili kujitangaza kwa wateja.

“Na tumewaelekeza hawa wafanyabiashara kuuza nyama choma kwa bei rafiki ambayo kila mtu ataweza kuimudu,” ameongeza.

Tamasha hilo limeandaliwa na DC Surumbu kwa lengo la kutangaza fursa za biashara zilizopo, ikiwemo nyama choma ya mifugo inayopatikana katika wilaya ya Tarime na mkoa wa mara kwa ujumla.

DAS Mwaisenye amefafanua kuwa walengwa katika biashara hiyo ya nyama choma, ni pamoja na watalii wanaotua katika Uwanja Mdogo wa Ndege Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime, kabla ya kuelekea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

“Tunahitaji wageni wakishuka hapa Tarime, kabla ya kwenda kutembelea Hifadhi ya Serengeti kupitia lango la Lamai, wapate nyama laini na bora ya kuchoma,” amesema.

Mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo ni la kwanza kufanyika wilayani Tarime, anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kwa mujibu wa DAS Mwaisenye.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages