Na Mwandishi Wetu
--------------------------
Katika harakati za kujikwamua kiuchumi, wakazi wa Musoma Vijijini waliojiunga pamoja kiushirika wameanzisha mradi wa ufugaji samaki kwa kutumia vizimba ndani ya Ziwa Victoria.
Chini ya uongozi wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi wa Kitongoji cha Busumi, wavuvi hao wamefanikiwa kupata mkopo nafuu wa shilingi milioni 117 kutoka serikalini ili ziwasaidie kupata vizimba vinne, vifaranga vya samaki, chakula na bima ya ufugaji.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini iliyotolewa jana, tayari wataalam wa usukaji vizimba wamekamilisha kazi na kuvipeleka ndani ya Ziwa Victoria eneo la Suguti.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uvuvi wa vizimba jimbo la Musoma Vijijini umeanza kwa mafanikio katika vijiji vya Kigera, Kwai Kwitururu na Suguti.
Imeelezwa kwamba wavuvi wa maeneo mengine wamehamasika na wanajiandaa kutuma maombi ya mkopo serikalini kwa ajili kushiriki katika uvuvi wa vizimba.
Wavuvi ambao tayari wameshaneemeka kwa mikopo wameishukuru serikali kwa kuboresha aina ya ufugaji wao uwe wa kisasa na wenye tija.
No comments:
Post a Comment