NEWS

Tuesday, 20 August 2024

Barrick North Mara wavipatia vijiji vitano gawio la mrahaba, Waziri wa Madini atoa maelekezo



Walioshikilia hundi za mfano ni viongozi wa vijiji vitano wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, Barrick na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wilayani Tarime leo Agosti 20, 2024.
-----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------

Vijiji vitano vilivyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, vimepokea gawio la mrahaba wa shilingi bilioni 2.365 zilizotolewa na mgodi huo kwa nyakati tofauti.

Kati ya kiasi hicho cha fedha, shilingi bilioni 1.224 ni malipo ya robo ya pili ya mwaka 2023 na robo ya kwanza ya mwaka 2024, wakati shilingi bilioni 1.141 ni malipo ya robo ya pili ya mwaka 2024, yaliyotokana na asilimia moja ya uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo.

Hundi za mfano zenye thamani ya shilingi bilioni 1.141 zimekabidhiwa kwa viongozi wa vijiji hivyo leo Agosti 20, 2024, katika hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo, kilomita chache kutoka mgodini hapo.

Vijiji hivyo na kiasi cha fedha zilizopokewa zikiwa kwenye mabano ni Kerende (401,450,317), Nyangoto (257,803,343), Nyamwaga (200,977,254), Genkuru (197,411,877) na Kewanja (83,450,153).

Viongozi wa vijiji hivyo wamekabidhiwa hundi hizo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde mbele ya viongozi mbalimbali wa serikali, jamii na Kampuni ya Barrick Gold inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Katika hotuba yake, Waziri Mavunde amewaelekeza viongozi wa wilaya, kata na vijiji husika kuhakikisha fedha hizo zinatumika kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa wananchi.

“Lengo letu [serikali] ni kuona wananchi wananufaika na shughuli hizi [uchimbaji madini), hivyo fedha hizi zitumike kugharimia utekelezaji wa miradi itakayoleta matokeo chanya, ili wananchi waone manufaa ya mgodi huu,” amesisitiza.

Aidha, Waziri Mavunde ameupongeza mgodi wa North Mara kwa kutoa gawio hilo kwa uwazi na kutaka fedha hizo kuibua miradi ambayo itasaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika vijiji hivyo.

“Naupongeza mgodi wa North Mara kwa kulifanya hili kwa uwazi. Pesa hizi ni nyingi zikitumika vizuri zitaleta manufaa kwenye vijiji vitano,” Waziri Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi gawio la robo ya pili ya mwaka 2024 amesema.

Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Madini, Masache Njelu Kasaka ameipongeza Barrick North Mara kwa kutekeleza maelekezo ya serikali ya kutoa gawio la mrahaba kwa uwazi.

“Kama Bunge tunaupongeza mgodi kufanyia kazi ushauri tulioutoa, leo mrahaba unatolewa kwa uwazi. Tutaendelea kuishauri serikali kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati,” amesema Njero.

Kwa upande wake Mkuu mpya wa Wilaya ya Tarime, Maja Edward Flowin Gowele amesema moja ya majukumu yake itakuwa kuhakikisha kwamba mapato yanayotokana na mgodi huo yanatumika vizuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Makabidhiano ya hundi
--------------------------------

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido amesisitiza umuhimu wa mashirikiano katika kutatua changamoto za wananchi.

“Tunahitaji kushirikiana na kutatua changamoto kwa jamii ili kuwa na uzalishaji endelevu,” amesema Dkt Ngido.

Ametumia nafasi hiyo pia kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

“Nitoe shukrani zetu [Barrick] kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Tunaona mwanga zaidi,” amesema Dkt Ngido.

Mapema, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko amemueleza Waziri Mavunde kuwa vijiji vilivyopewa malipo hayo ni ambavyo vilikuwa na haki ya kuchimba madini kwenye simo la Nyabigena.

“Baada ya Kampuni ya Barrick kuchukua dhamana ya uendeshaji wa mgodi mwaka 2019 chini ya ubia wa Twiga, ilirejea kufanya tafiti za kijiolojia katika shimo la Nyabigena na kufanikiwa kuanza tena uzalishaji kwenye robo ya pili ya mwaka 2023 baada ya kusimama tangu mwaka 2017.

“Hii ina maana kwamba vijiji tajwa vimeendelea kupata gawio la mrahaba kama ilivyokuwa awali. Hii hufanyika kila robo ya mwaka kutokana na hali ya uzalishaji na uuzaji wa dhahabu,” amesema Lyambiko.

Viongozi wa vijiji hivyo wameahidi kwenda kushirikisha wananchi katika uibuaji wa miradi itakayogharimiwa na fedha hizo za mrahaba.

“Sisi katika kijiji chetu tunatarajia kutumia fedha tulizopata kugharimia ukamilishaji wa soko jipya la Nyangoto, ukarabati wa barabara na miradi mingine,” amesema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwita Mosegi.
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages